Featured Kitaifa

KAMATI YA BUNGE YATAKA KIKOSI MAALUM KUPAMBANA NA UKATILI WA KIJINSIA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt Dorothy Gwajima akiwasilisha utekelezaji wa Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa Fedha 2021/2022 na makadirio ya Mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii jijini Dodoma tarehe 25/03/2022.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya  Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Stanslaus Nyongo akieleza jambo kwa uongozi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum wakati wa kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika jijini Dodoma tarehe 25/03/2022 Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Zainab Chaula akifafanua jambo wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kilichofanyika jijini Dodoma tarehe 25/03/2022  

Baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum wakifuatilia kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kilichofanyika jijini Dodoma tarehe 25/03/2022. 

Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WMJJWM

…………………………………………………..

Na WMJJWM-Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeitaka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kuja na wazo la kuanzisha kikosi Maalum cha kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia nchini.

Hayo yamesemwa leo tarehe 25/03/2022 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Stanslaus Nyongo wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu na Bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/22 na makadirio  ya mapato na matumizi kwa mwaka 2022/23. 

Mhe.  Nyongo amesema kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku, hivyo jitihada thabiti zinatakiwa kuchukuliwa ili kuhakikisha jamii inaepukana na vitendo hivyo kwa kuwa na Mpango dhabiti wa kupambana na tatizo hilo.

“Mimi naona kwa mfano mapambano dhidi ya mauaji ya wanyama kumeundwa Jeshi usu kwanini Wizara isishawishi kuwe na Kikosi Maalum kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwani ni janga pia kubwa linaangamiza Jamii yetu na watu wetu” amesema Mhe. Nyongo

Aidha amemtaka Waziri Dkt. Gwajima kuisimamia Wizara katika utekelezaji wa majukumu yake kwakuwa ameaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo kuwa mbunifu pamoja na Menejimenti yake ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuleta tija kwenye jamii ya watanzania

Akiwasilisha taarifa ya majukumu , utekelezaji wa Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2021/22 na makadirio ya Mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/23 Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt Dorothy Gwajima amesema, Wizara imejipanga katika kuhakikisha inaihudumia jamii hasa katika kutoa elimu mbalimbali ili kujikwamua kiuchumi na kupambana na changamoto ikiwemo ukatili wa kijinsia.

Ameongeza kuwa Wizara imeimarisha uratibu na usimamizi wa shughuli za wafanyabiashara ndogo ndogo,  Machinga kufuatia maelekezo ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyotoa tarehe 25 Januari 2022 kwamba Serikali inawatambua machinga wote nchini kama kundi maalum ambalo litakuwa chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. 

“Kufuatia maelekezo hayo uongozi wa Wizara ulipokea rasmi na kukutana na viongozi wa Shirikisho la Umoja wa Machinga (SHIUMA) Taifa tarehe 27 Januari 2022 na 24 – 27 Februari 2022 na kubaini kuwa Shirikisho hilo halikuwa na usajili, anwani, ofisi ya kitaifa ya kufanyia kazi, mgogoro baina ya viongozi na kukosekana kwa kanzidata ya taarifa za Machinga” amesema Dkt. Gwajima 

Dkt. Gwajima amesema kuwa upande wa Haki na Maendeleo ya Mtoto na kukabiliana na ukatili dhidi ya watoto wa kike nchini, Wizara imezindua Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Ukeketaji unaotekelezwa kwa kipindi cha mwaka 2020/21 – 2024/25 uliozinduliwa mwezi Novemba, 2021.

Amesisitiza kuwa Wizara imeratibu uundwaji wa Muungano wa Wadau  watakaosimamia na kutekeleza afua za kupinga vitendo vya ukeketaji nchini (Anti-FGM Coalition) na  Muungano huo unajumuisha watendaji wa Wizara za Kisekta na Wadau wa Maendeleo.  

Pia ameeleza kuwa katika kutekeleza ajenda ya usawa wa kijinsia, Wizara ilifanya uzinduzi wa Kamati ya Ushauri ya Kitaifa ya Utekelezaji wa Ahadi za Nchi kuhusu Kizazi Chenye Usawa (Generation Equality Forum – GEF)   iliyozinduliwa tarehe 16 Disemba, 2021 na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Akifafanua jambo katika kikao hicho Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula amesema Wizara inashirikiana na wadau katika kuhakikisha wanatekeleza afua mbalimbali ndani ya jamii ikiwemo kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto.

About the author

mzalendoeditor