Featured Kitaifa

UBOMOAJI NYUMBA MSIMBAZI BONDENI KUANZA RASMI APRILI 12, 2024

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Zoezi la ubomoaji wa nyumba zilizofidiwa na Mradi wa Uendelezaji wa Bonde la Msimbazi linatarajiwa kuanza rasmi Aprili 12, 2024, na litawahusu waathirika 2,155 ambao tayari wamelipwa fidia.

Hayo yamesemwa na Mhandisi Humphrey Kanyenye, Mratibu wa Miradi ya Ushirikiano na Benki ya Dunia TARURA alipokuwa akiongea na waandishi wa habari katika ofisi za mradi zilizopo Millenium Tower-Kijitonyama, Dar es Salaam.

Mhadisi Kanyenye alieleza kuwa kwa mujibu wa makubaliano ya utekelezaji wa zoezi hilo, waathirika wa mradi ambao wameshakwishapokea malipo yao wanatakiwa kuhamisha mali zao na kupisha eneo la mradi ndani ya wiki sita (6) baada ya kupokea fedha hizo kwenye akaunti zao.

“Waathrika wote wa mradi huu wanafahamu kuwa tuliwapa muda wa kuhama kwa makubaliano maalumu ya kimkataba yaliyowataka kuhama ndani ya wiki Sita (6) mara tu baada ya fedha kuingia katika akaunti zao, muda huo sasa umepita hivyo wanatakiwa kuondoka ili kupisha utekelezaji wa mradi,” alisema Mhandisi Kanyenye.

Alieleza pia kuwa walichelewa kuanza zoezi hilo kwa ajili ya kuwapa muda waathirika wa mradi kubomoa wenyewe kwa hiari ili kuokoa baadhi ya mali zao.

Aidha, alisema kwamba kati ya waathirika 2,329 waliopo kwenye orodha ya daftari la kwanza la ulipaji fidia, kufikia tarehe 21 Machi 2024, tayari waathirika 2,151 walikuwa wamelipwa kiasi cha shilingi bilioni 52.6

“Lakini pia kuna wale ambao hawakufikiwa katika uthamini wa awali kwa baadhi yao kugomea ama kutoonekana katika maeneo yao, idadi yao ni 466, hawa wameingizwa katika orodha ya daftari la pili ambalo limeshakamilika na litawasilishwa kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kusainiwa siku ya jumanne tarehe 26 Machi 2024 tayari kwa kulipwa fidia,” alisema Mhandisi Kanyeye.

Mradi unatekelezwa kwa muda wa miaka sita (6) (2022-2028) kwa gharama takribani shilingi bilioni 663 na lengo kuu la mradi ni kuimarisha ustahimilivu kwa kuweka mikakati ya kukabiliana na mafuriko na kuwa na matumizi bora ya ardhi katika eneo la chini la bonde la mto msimbazi ikiwa ni pamoja na kurudisha uoto wa asili katika uwanda wa juu wa bonde la mto msimbazi.

About the author

mzalendo