Featured Kitaifa

DKT.DIMWA : ATOA MKONO WA POLE KWA FAMILIA ZA MAKADA WA CCM WALIOFARIKI PEMBA

Written by mzalendo

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,akizungumza katika ziara yake ya kuifariji na kutoa mkono wa pole kwa familia ya Katibu mstaafu wa Siasa na Uenezi  CCM Mkoa wa Kusini Pemba marehemu Mwl Khatib Haji Khalid,aliyefariki hivi karibuni huko Jimbo la Kiwani Mkoa wa Kusini Pemba.

NA IS-HAKA OMAR,PEMBA.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt Mohamed Said Dimwa,ametoa mkono wa pole na kuzifariji familia za Viongozi na Makada wa CCM waliofariki Dunia siku za hivi karibuni katika maeneo mbali mbali ya Kisiwa cha Pemba.

Kupitia ziara hiyo Dkt.Dimwa amewasihi,ndugu wa familia,marafiki na jamaa wa karibu kuendelea kuwa wavumilivu na wawaombee dua ndugu zao waliofariki ili wawe na makaazi mema katika pepo ya Mwenyezi Mungu.

Amesema Chama Cha Mapinduzi kilipokea kwa majonzi na mshituko mkubwa taarifa za vifo hivyo vilivyowapoteza makada waliokuwa mstari wa mbele katika kulinda,kutetea na kusimamka kwa vitendo maslahi ya CCM.

Katika ziara hiyo Dkt.Dimwa,alifika Jimbo la Kiwani kuifariji na kutoa mkono wa pole kwa familia ya aliyekuwa Katibu mstaafu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba Marehemu Mwl.Khatib Haji Khalid aliyeacha wajane wawili ambao ni Bi.Kazija Faki Abdalla na Bi.Mwanamiza Jape Khatib na kueleza kuwa CCM itaendeleza kuwa karibu na familia hiyo katika masuala ya Kijamii.

Wakati huo huo alitoa mkono wa pole kwa familia ya aliyekuwa kada wa CCM Tawi la Ukutini Jimbo la Chambani, Marehemu Hassan Ali Faki na kuwasihi waendelee kuwa wavumilivu na wamuombee dua nyingi kada huyo.

“Tumepoteza nguvu kazi na watu muhimu sana waliojitolea kufanya mambo yenye tija ndani ya Chama chetu hivyo nasaha zangu kitu pekee cha kuwalipa ni kuwaombea dua nyingi Mwenyezi Mungu awajaalie nafasi katika pepo ya Firidausi”,alieleza Dkt.Dimwa.

Amewaka Wanachama wa CCM nchini kuenzi kwa vitendo historia nzuri za kiutendaji,uadilifu,misimamo na uaminifu usiyoyumba ulioasisiwa na makada hao katika kukitumikia Chama na Jumuiya zake.

Katika maelezo yake Naibu huyo Dkt.Dimwa,alitoa wito kwa waumini wa dini ya kiislamu nchini kutumia vizuri fursa ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kufanya ibada,kutoa sadaka na kuwaombea dua ndugu na jamii waliofariki.

About the author

mzalendo