Na. Gideon Gregory, Dodoma.
Chama Cha Wafugaji Tanzania (CCWT) kimetangaza muda wa kuchukua fomu za kugombea nafasi za uongozi kwa wanachama wake wanaotaka kugombea huku wakibainisha kuwa malipo ya uchukuaji wa fomu hizo yanapaswa kufanyika kupitia akaunti ya tume ya uchaguzi na sio kwenye akaunti ya chama hicho.
Hayo yameelezwa leo Machi 12, 2024 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi ya CCWT Bw. Charles Lyuba alipokutana na waandishi wa habari katika ofisi ya chama hicho ambapo amesema kuwa lisiti za malipo zinapaswa kuambatanishwa katika fomu wakati wa kuzirejesha.
“Tangu mwaka jana tumeanza mchakato wa uchaguzi na hadi sasa tunaendelea na chaguzi za ngazi mbalimbali ikiwemo za wilaya, nawatangazia wafugaji na wanachama wote kuwa fomu za kugombea uongozi ndani ya chama chetu ngazi ya kanda na taifa zitaanza kutolewa Machi 13 – 25,2024 na mwanachama yeyote mwenye nia ya kugombea nafasi yeyote ya kanda anapaswa kuzingatia ratiba na kalenda nzima inayotolewa na tume,”amesema.
Amesema wanachama wao ni muhimu kuwa na taarifa sahihi zinazohusu uchaguzi ili kuepuka mikanganyiko na hasa wanapotoa ratiba isije kuonekana kuna watu wana ratiba zao binafsi.
“Hii ndio ratiba ya tume ya uchaguzi na sisi tunasema hiyo tarehe 13 kwa maana ya kesho hadi tarehe hadi tarehe 25, Machi tunaanza kutoa hizo fomu za kanda sambamba na fomu za ngazi ya taifa,” amesema.
Aidha Bw. Lyuba amewasisitiza wagombea wote kufuata ratiba ya tume ipasavyo na kuchukua fomu kwa wakati kwa ngazi ya taifa uchaguzi utaanza Aprili 8,2024 utakao wahusisha viongozi wote wa wilaya na walaya ambayo haitakuwa imefanya uchaguzi wa ngazi haitaruhusiwa kufanya uchaguzi wa ngazi ya kanda pamoja na taifa kwasababu watakuwa hawajatimiza takwa la katiba ya wanachama hicho.
Kwa upande wake mjumbe wa tume ya uchaguzi George Kifuliko amewasisitiza wagombea na wanachama wote kuzingatia ratiba ili kuepusha vikwazo vitakavyojitokeza.