Kitaifa

C FM YAADHIMISHA MSIMU WA NNE WA MWANAMKE MWAMBA 2024

Written by mzalendo

Na. Gideon Gregory, Dodoma.

Kamishna Msaidizi Idara ya Undelezaji wa Sekta ya Fedha Bi. Janeth Lewis Hiza amewataka Wanawake kuwekeza fedha wanazozipata katika njia mbalimbali za mapato ili waweze kupata mitaji na kufungua Biashara zitakazo wasaidia huko mbeleni.

Bi.Janeth ametoa wito huo Machi 10,2024 Jijini Dodoma alipokuwa kwenye hafla ya ‘MWANAMKE MWAMBA’ msimu wa nne ulio asisiwa na kituo Cha redio Cha C fm 103.3, ikiwa ni katika kusherehekea siku ya Wanawake Duniani.

“Zamani tulikuwa tunategemea kilimo tu ili kuweza kupata fedha, lakini siku hizi tunatafuta pesa kwa njia mbalimbali ikiwemo kilimo, hivyo nikusihi wewe mama, Usile fedha yako yote unayoipata, jitahidi kuwekeza na Baadae hizo fedha uende kuweka Benki ili ziweze kuzaa na wewe kupata mtaji nk.” alisema.

Bi.Janeth amesema wanawake hao hawapaswi kujidharau kwani kuna Hazina kubwa waliyopendelewa na Mungu hivyo wanapaswa kufanya jambo ambalo wameletwa duniani kuja kulifanya kwa juhudi na maarifa.

Aidha, amesema kuwa katika nchi yetu ya Tanzania kuna fursa nyingi sana hivyo amewataka wanawake hao kuchangamkia fursa hizo za mikopo kwa kuanzisha vikundi, vikasajiliwa na kusimamiwa na benki kuu ili waweze kufikia malengo yao.

“Hakuna kitu kizuri kama kuwa kwenye Kikundi mpaka ndugu zetu wa PPRA wanatambua vikundi, wakawapa miradi. kwahiyo wakina mama wenzangu tafuteni Marafiki watano waaminifu ili muweze kutumia hizo fursa, Mimi nipo tayari kuwasapoti” alisema Bi.Janeth.

Pia amewashawishi wakinamama hao kufungua vituo vya kulelea watoto(Day Care) ili waweze kusaidia kwenye suala la malezi bora kwa watoto.

Naye Mama mlezi wa kituo hicho cha Redio Mama Tunu Pinda, amewapongeza Wanawake wote walioshinda tuzo ya ‘Mwanamke Mwamba’ kwa Mwaka huu 2024 na kwa wale ambao hawakushinda,amewataka wasikate tamaa kwani hata mwaka ujao wanaweza kushinda pia.

Kwa upande wake Mkuu wa vipindi C-Fm 103.3 Bw.James Mbonde amesema dhumuni la siku ya ‘Mwanamke Mwamba’ ni kumpa thamani Mwanamke, kumshika mkono, pamoja na kumtia moyo kwa jitihada mbalimbali ambazo amekuwa akizifanya katika maendeleo ya Jamii na taifa kwa ujumla.

“Sisi Kama kituo Cha Burudani Kanda ya kati na kuelimisha Jamii, tunaamini nguvu ya Mwanamke na mchango wake katika Jamii, na kwa kulithibitisha hilo tumekuwa mstari wa mbele kutumia nguvu na uwezo tulionao kutoa elimu pamoja na kufungua fursa mbalimbali kwa Mwanamke wa Kanda ya kati, pamoja na kuwasaidia baadhi ya Wanawake wenye changamoto mbalimbali na kuwainua kiuchumi,” amesema.

Naye Mwanamke Mwamba Bi.Anjella Layzer aliyeshinda tuzo ya Mwanamke Mwamba katika kipengele Cha ‘Mwamba Katika Chakula’ amesema tuzo hiyo aliyoishinda ina maana kubwa sana katika maisha yake na imempa hamasa ya kupambana zaidi katika kitu anachokifanya.

 

About the author

mzalendo