Na.Mwandishi Wetu-ZANZIBAR
VYOMBO vya habari vimetakiwa kuwa mstari wa mbele kuanisha changamoto za kiuchumi na kifedha zinazoikabili jamii ili zipatiwe ufumbuzi na taasisi za kifedha.
Akizungumza katika kikao maalum na uongozi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), Meneja wa biashara wa benki ya CRDB Zanzibar, Abdalla Duchi, alieleza kuna changamoto ya uhaba wa elimu ya kifedha katika jamii jambo linalopelekea kuzorota kwa shughuli za maendeleo.
Alieleza kuwa pamoja na juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhimiza ujasiriamali na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, bado elimu jumuishi ya kifedha inahitajika ili kuwe na matokeo chanya.
Aidha Duchi aliahidi kuendelea kutumia vyombo vya habari na waandishi wa habari kueleza shughuli zinazofanywa na benki hiyo, hivyo aliwataka wanahabari kuendelea kushirikiana nao kusambaza elimu kwa umma.
“Niwapongeze kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuelimuisha jamii juu ya masuala yanayohusu ustawi wao kiuchumi na kijamii jambo linalopaswa kufanywa kwa kasi zaidi kwa mashirikiano tunayoyaanzisha leo”, alieleza Duchi.
Alifafanua kuwa benki hiyo ina huduma mbali mbali zinazowagusa wananchi wa ngazi zote ikiwemo akaunti ya kiislamu Al Barakah na bima mbali mbali zinazoweza kuwanufaisha wateja pindi wanapopatwa na majanga, misiba au ulemavu.
“Miongoni mwa bidhaa tulizonazo ni bima ya mtu mmoja mmoja na ya vikundi ambayo hutoa mafao yasiyopungua shilingi milioni moja kwa ajali, kifo, majanga, ulemavu wa kudumu, elimu na kadhalika kwa gharama inayoanzia shilingi 1,000”, alieeleza Meneja huyo.
Awali Mwenyekiti wa ZPC, Abdallah Mfaume, alieleza lengo la ziara hiyo inayofanyika kila mwanzo wa mwaka ni kuimarisha mahusiano baina ya klabu na wadau wake.
Alieleza kuwa ZPC ni taasisi mwamvuli wa waandishi wa habari wanaoishi na kufanya kazi katika vyombo mbali vya habari vya ndani na nje ya Zanzibar ikiwa na jukumu la kuwaunganisha kitaaluma ili kujenga weledi wanachama wake kupitia shughuli mbali mbali.
Aliongeza kuwa katika kutekeleza majukumu yake, ZPC hutoa mafunzo yanayowajengea uwezo wanachama wake na waandishi wa habari hivyo kukua kwa mahusiano baina yake na benki hiyo kutaongeza uelewa wa jamii na wanachama wa klabu juu ya masuala ya kifedha na njia za kujiongezea kipato.
“Tumekuwa na utaratibu huu kila mwaka lengo ni kukumbushana juu ya namna bora ya kufanya kazi pamoja kwa malengo ya kukuza ufanisi wa malengo tuliyojiwekea kupitia shughuli za taasisi zetu”, alieleza Mfaume.
Kwa upande wake Meneja Biashara wa benki ya Kiislamu wa CRDB Zanzibar, Anwar Said, alieleza kufurahishwa kwake na ziara ya viongozi hao na kuongeza kuwa benki hiyo inaendelea kutoa huduma mbali mbali kupitia akaunti ya Al Barakah toka ilipoanzishwa mwezi Novemba 2021.
“Katika benki ya kiislamu kuna huduma na bidhaa nyingi sana ikilinganishwa na benki nyengine ambazo tutahitaji msaada wa vyombo vya habari kuujulisha umma”, alieleza Anwar.
Katika ziara hiyo Mfaume aliambatana na Katibu Mkuu wa Zpc, Mwinyimvua Nzukwi, Mjumbe wa Kamati Tendaji, Zuhura Msabaha na Mratibu, Mgeni Hamad wakati mbali ya Duchi na Anwar, CRDB iliwakilishwa na Afisa Biashara na Mauzo, Lucy Mbuya na Afisa Ubora wa huduma, Zainab Ally.