Featured Kitaifa

KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA JKCI KWA KUENDELEA KUTOA HUDUMA BORA

Written by mzalendoeditor

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imeipongeza na kuitaka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuendelea kutoa huduma bora za matibabu ya kibingwa na kuwa Kituo mahiri kwenye utoaji wa matibabu ya moyo katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki.

Pongezi hizo zimetolewa leo na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dkt. Faustine Ndugulile leo Februari 21,2024 wakati wa ziara ya kutembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Jijini Dar Es Salaam kuona hali ya utoaji Huduma kwa wananchi pamoja na ukaguzi wa miradi ya Afya katika Taasisi hiyo.

Dkt. Ndungulile amesema kunahaja kubwa ya kuhakikisha Taasisi hiyo inatanua wigo wa Huduma hizo katika kanda na mikoa mingine ili kupunguza misongamano ya wananchi na kuruhusu wigo mpana wa upatikanaji wa Huduma hizo kwa wingi nchini.

“ Kwa kutanua wigo kwa kufungua matawi ya Taasisi hii katika kanda na mikoa nchini itasaidia kuokoa gharama za usafiri kwa wananchi, kupatiwa huduma kwa wakati kabla ya maradhi hayajawa makubwa”, amesisitiza Dkt. Ndungulile.
Vile vile ametoa wito kwa Taasisi hiyo kuendelea kutoa elimu juu ya matatizo ya moyo kwa wananchi ili kuwa na uelewa wa matatizo ya moyo na kuwahi matibabu kwa wakati.

Kamati hiyo imepokelewa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Bw. Tumainieli Macha, pamoja na watumishi wengine wa Wizara pamoja JKCI

About the author

mzalendoeditor