SERIKALI kupitia Wizara ya Maji imesema imekuwa ikitenga fedha za utekelezaji wa Mradi wa Maji Mageri utakaohudumia Vijiji nane vya Tinaga, Oloirien, Ngarwa, Yasi, Mdito, Mageri, Mugongo na Magaiduru Wilayani Ngorongoro Mkoani Arusha ambapo hadi sasa jumla ya Shilingi 2,264,520,000.00 zimetolewa.
Hayo yamesemwa leo Februari 5 2024 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati akijibu swali la mbunge wa Ngorongoro Emmanuel Shangai ambae aliuliza ni lini Serikali itatenga fedha za kutosha kwa ajili ya kumaliza Mradi wa Maji Mageri utakaohudumia Vijiji nane Wilayani Ngorongoro.
Mhandisi Mahundi amesema Fedha hizo zimesaidia kukamilisha utekelezaji wa banio la chanzo cha maji Orkanjor, ulazaji wa bomba kuu kutoka kwenye chanzo hadi kwenye tenki umbali wa Kilometa 3 na ununuzi wa pampu 2 zenye uwezo wa kusukuma maji lita 2,054,400 kwa Siku.
“Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zinazoendelea kwa sasa ni pamoja na ujenzi wa matenki Tisa (9) yenye jumla ya ujazo wa lita 2,000,000, uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa mabomba ya usambazaji umbali wa Kilometa 80. Aidha, utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa asilimia 40 na unatarajiwa kukamilika Mwezi Desemba, 2024″amesema Mahundi