Kitaifa

THBUB KUFUATILIA HAKI ZA WAFANYAKAZI KATIKA MAKAMPUNI YA ULINZI

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), inatarajia kufanya ufuatiliaji kuhusu utekelezaji wa haki za wafanyakazi na viwango vya ajira sehemu za kazi ambapo ufuatiliaji huo unatarajiwa kufanyika katika mikoa ya Iringa, Dar es Salaam na Kagera na utahusisha makampuni binafsi ya ulinzi kuanzia Februari 5 – 10,2024.

Hayo yamebainishwa leo Februari 2,2024 Jijini Dodoma na Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari.

Amesema kazi hiyo inalenga kufuatilia utekelezaji wa Sheria na Kanuni zinazoyataka makampuni ya aina zote kutekeleza majukumu yao kwa kuheshimu haki za binadamu na upatikanaji wa suluhisho na fidia kwa wahanga wa ukiukwaji wa haki hizo unaohusishwa na shughuli za kibiashara au uwekezaji.

“Hivyo, miongoni mwa maeneo yatakayoangaliwa katika ufuatiliaji huo ni pamoja na Mikataba ya ajira, iwapo inakidhi viwango vya ajira; afya na usalama kazini; na utunzaji wa taarifa binafsi za waajiriwa,”amesema.

Sambamba na hayo maeongeza kuwa maeneo yatakayo angaliwa ni uwepo wa vyama vya wafanyakazi, mahusiano ya makampuni ya ulinzi na jamii, na stahiki nyingine wanazopaswa waajiri kutoa kwa wafanyakazi wao.

“Baada ya ufuatiliaji huo, Tume itatoa taarifa yenye mapendekezo ya namna ya kuboresha uzingatiaji wa haki za wafanyakazi na viwango vya ajira katika makampuni binafsi ya ulinzi,”amesema.

Mwaimu amesema utekelezaji wa kazi hiyo ni mwendelezo wa ufuatiliaji wa masuala ya biashara na haki za binadamu nchini na kutoa mfano kuwa Mwezi Desemba 2023 tume ilifanya tathimini ya utendaji kazi kwa taasisi zisizo za kimahakama zinazoshughulikia malalamiko na migogoro inayohusiana na masuala ya biashara na haki za binadamu. 

“Tume inatoa shukrani zake za dhati kwa Serikali kwa kuipatia mazingira wezeshi kutekeleza majukumu yake, na kwa Taasisi ya Haki za Binadamu nchini Denmark (Danish Institute for Human Rights – DIHR) kwa kuiwezesha kiufundi na kirasilimali kufanikisha utekelezaji wa kazi hii na nyingine zilizotangulia,”amesema.

About the author

mzalendo