Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizindua Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii katika hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam tarehe 31 Januari 2024.
…………..
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amezielekeza Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Mamlaka nyingine zinazohusika kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi madhubuti wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ili uweze kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii uliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Amesema ni lazima kuweka mfumo mzuri wa uratibu wa shughuli za mpango huo na kuhakikisha taarifa za utekelezaji zinapatikana ikiwemo kutumia mifano ya kidijitali.
Makamu wa Rais amewasihi wahudumu wa afya watakaopewa dhamana ya kutekeleza jukumu hilo kuzingatia weledi na kujituma pamoja na kutoa rai kwa jamii kuupokea mpango huo na kuthamini huduma za wahudumu wa afya ngazi ya jamii kwa kuwapa ushirikiano wa kutosha ili kulinda na kuboresha afya katika jamii.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesisitiza masuala ya lishe bora na usafi wa mazingira yasiachwe nyuma katika kutekeleza Mpango huo kama njia mojawapo ya kujenga afya na kudhibiti magonjwa ambayo yanatokana na uchafuzi wa mazingira ikiwemo kipindupindu na malaria. Ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa, Wadau wa Maendeleo na Wadau wengine kuunga mkono juhudi za Serikali pamoja na vipaumbele vya Mpango huo vilivyoainishwa wakati wote wa utekelezaji.
Vilevile Makamu wa Rais amewasihi viongozi wote wanaohusika katika ngazi zote kuhakikisha zoezi la kuwachagua Wahudumu wa afya ngazi ya jamii linafanyika kwa kufuata vigezo na taratibu zilizowekwa ili kupata Wahudumu wenye sifa stahiki watakaotekeleza majukumu hayo. Amewataka watakaopewa jukumu la kutekeleza mpango huo, kujiepusha na vitendo vya upendeleo, rushwa au ukiukwaji wa taratibu.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imepanga kuajiri na kuwajengea uwezo jumla ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wapatao 137,294 katika Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara ambapo Utekelezaji wa Mpango huo utafanyika katika kipindi cha miaka mitano kwa awamu ambapo katika mwaka wa kwanza (2023/24) zaidi ya Wahudumu 28,000 watafikiwa na baadaye wastani wa Wahudumu 27,324 kila mwaka kwa kipindi cha miaka minne mfululizo kuanzia mwaka 2024/25 hadi 2027/28. Jumla ya shilingi bilioni 899.4 zinatarajiwa kutumika katika kutekeleza mpango huo kwa kipindi cha miaka mitano.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema Mpango huo umelenga kupunguza idadi ya wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa kuimarisha huduma za afya kinga pamoja na kuongeza tija na ufanisi katika kutoa huduma za afya kufikia lengo la afya kwa wote.
Ameongeza kwamba Mpango huo utasaidia kukabiliana na upungufu wa vituo vya kutolea za afya hususani katika maeneo ya vijijini. Aidha amesema kupitia mpango huo wahudumu wa afya ngazi ya jamii wameweza kuibua magonjwa mbalimbali yanayoikabili jamii kama vile Kifua Kikuu, Kipundupindu na ugonjwa wa Marburg.
Amesema kupitia mpango huo wataweza kupunguza gharama za matibabu kutokana na kutambulika kwa ugonjwa katika hatua za awali zaidi. Amesema umuhimu wa wahudumu hao ngazi ya jamii ni daraja kati ya vituo vya kutolea huduma na jamii husika kwa kuwa wamekuwa wakitambua mapema maradhi yanayojitokeza.
Waziri Ummy amesema katika kuchagua wahudumu wa afya ngazi ya jamii suala la wakazi wa eneo husika litazingatiwa ili kuendana na mila na desturi za wananchi wa eneo hilo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam kuzindua Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii. Tarehe 31 Januari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Uzinduzi wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam tarehe 31 Januari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizindua Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii katika hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam tarehe 31 Januari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikata utepe kuashiria kuzindua kitabu cha Muongozo wa Utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mpango huo iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam tarehe 31 Januari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwakabidhi baadhi ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kitabu cha Muongozo wa Utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mpango huo uliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam tarehe 31 Januari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akipokea tuzo maalum ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyotolewa na Sekta ya Afya wakati wa uzinduzi wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii katika hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam tarehe 31 Januari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wahudumu wa afya ngazi ya jamii mara baada ya kuzindua Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii katika hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam tarehe 31 Januari 2024.