Kitaifa

EWURA CCC YAELEKEZWA KUTAFUTA VYANZO VYA FEDHA

Written by mzalendo


Na. Gideon Gregory, Morogoro.

Mamlaka ya udhibiti wa huduma za Nishati na Maji (EWURA) imelielekeza Baraza la ushauri la watumiaji wa huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC) kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha ili kuziwezesha Kamati za mikoa kupanua wigo kwa kuwafika wananchi wa pembezoni kuwaelimisha namna ya kuwasilisha malalamiko yao pindi wanaposhindwa kupata huduma zenye ubora.

Aidha imeliekeza Baraza hilo kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Kamati hizo ili ziweze kutekeleza vyema majukumu yake na kueleza kuwa ikiwa kuna changamoto za kiutendaji Baraza linapaswa kuwasiliana na mdhibiti kuona namna ya kuzitatua.

Hayo yameelezwa leo mkoani Morogoro na Meneja wa EWURA Kanda ya Mashariki Mhandisi Musira Nyirabu wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati za mikoa na kuwataka wajumbe hao kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao kwa kujitoa kwa dhati kufikia vipaumbele vya kiutendaji.

Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu,Mamlaka ya udhibiti wa huduma za Nishati na Maji Dk. James Andilile,Mhandisi Nyirabu Aidha amelishauri Baraza kuyafanya mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe yakawe endelevu ili kuendana na wakati kutokana na mambo mengi kubadilika akitolea mfano wa urekebishwaji wa kanuni na kwamba bila kuendana na wakati wajumbe wanaweza kujikuta wakitumia taarifa zilizopitwa na wakati na kupotosha Umma.

“Kazi ya Wajumbe hawa ni kutetea watumiaji katika mikoa yao ambako ndiko watanzania wanaishi,hawa ni wawakilishi wa EWURA CCC katika mikoa yao, uwajibikaji na mshikamano wao ndiyo njia pekee itakayowezesha huduma za Nishati na Maji kuwa zenye ubora unaokubalika na watumiaji, “amesema.

Pia ametoa wito kwa watoa huduma za Nishati na Maji kote nchini zikiwemo Mamlaka za Maji, TANESCO pamoja na vituo vya mafuta ambao ni miongoni mwa wadau wakubwa wa Baraza kutoa ushirikiano wa dhati kwa Baraza na wajumbe wa Kamati za mikoa ili kutatua changamoto za wananchi kwa wakati.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa EWURA CCC Stella Lupimo amevitaja baadhi ya viashiria vya kiutendaji kwa wajumbe wa Kamati za mikoa kuwa ni pamoja na kuwajengea uelewa watumiaji kwa kutoa elimu kwa makundi 12 ya watumiaji huduma zinazodhibitiwa na EWURA kwa mwaka.

Vingine ni pamoja na kushiriki kwenye programu nne kwa mwaka za uelimishaji zenye ufadhili wa Baraza, kupokea malalamiko na kusaidia walalamikaji watumiaji angalau 20 wenye malalamiko na kuwaelekeza namna ya kulakamika, kufikia na kuelimisha wadau 1,480 kwa mwaka na kufuatilia utatuzi wa malalamiko hayo na kushiriki kuandaa taarifa za robo mwaka na kuiwakilisha kwa wakati.

Lupimo pia ametaja majukumu ya wajumbe hao kuwa ni kufanya mikutano na vikao vya kutathmini kazi, kuwa kiungo kati ya mtumiaji, baraza na Mdhibiti, kushiriki kwenye utatuzi wa malalamiko kwa mujibu wa kanuni, uwasilishaji na ushughulikiaji wa malalamiko ya EWURA na kuhamasisha Umma kushiriki na kuchukua hatua mbalimbali katika masuala ya udhibiti .

Amesema Baraza limefanikiwa kufungua Kamati 30 kwenye mikoa 26 kwa upande wa Tanzania bara, kuwajengea uwezo wajumbe wa Baraza, watumishi na wajumbe wa Kamati za mikoa, kutengeneza vitendea kazi na kufanya mikutano ya mwaka ya watumishi inayolenga kufanya tathmini ya kiutendaji na kuweka mipango kwa mwaka unaofuata.

Licha ya mafanikio hayo Kaimu Katibu Mtendaji huyo ameeleza changamoto zilizopo kwenye Baraza hilo kuwa ni utegemezi wa chanzo kimoja cha fedha kuendesha majukumu yake na kusababisha Baraza kushindwa kufungua Ofisi za mkoa kwa baadhi ya mikoa na kushindwa kuajiri.

EWURA CCC ilianzishwa chini ya kifungu Na. 30 cha sheria ya mamlaka ya udhibiti wa huduma za Nishati na Maji, sura ya 414 ili kutetea na kulinda maslahi ya watumiaji wa huduma hizo na ilianza rasmi kufanya kazi mwaka 2007 ambapo kimuundo inaongozwa na wajumbe wa Baraza wanaoteuliwa na Waziri mwenye dhamana .

About the author

mzalendo