Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akizungumza na Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian jijini Dar es Salaam tarehe 24 Novemba 2023.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (katikati) akizungumza na Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba jijini Dar es Salaam tarehe 24 Novemba 2023.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian pamoja na Watendaji kutoka Ubalozi huo, jijini Dar es Salaam tarehe 24 Novemba 2023.
……….
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Doto Biteko, leo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian ambapo walizungumza masuala mbalimbali ikiwemo uhusiano uliopo kati ya Tanzania na China na uwekezaji kwenye miradi
ya Nishati.
Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam tarehe 24 Novemba 2023 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Ubalozi wa China nchini Tanzania wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.
Dkt.Biteko, amemweleza Balozi Mingjian kuwa Tanzania inathamini uhusiano mzuri ulipo kati ya nchi hizi mbili ambao mwakani utafikia miaka 60 huku akitaja miradi mbalimbali kwenye Sekta ya Nishati na
Madini ambapo kuna Wawekezaji/Wakandarasi kutoka China.
“ Sisi Tanzania tunaufurahia na kuuthamini uhusiano mzuri uliopo na hapa kuna kampuni nyingi kutoka China zinazofanya kazi kwenye uchimbaji madini ikiwemo madini ya viwandani na uchenjuaji madini, pia kwenye miradi ya Nishati kuna kampuni za Kichina zinafanya kazi mfano kampuni ya TBEA inayojenga laini ya umeme ya kV 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma, na mradi wa kusafirisha umeme wa kV 400 kutoka Tanzania kwenda Zambia.” Amesema Dkt. Biteko
Kuhusu miradi hiyo ya usafirishaji umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma na mradi wa TAZA, Dkt. Biteko ametoa wito kwa Serikali ya China kuiwezesha kwa namna mbalimbali kampuni hiyo ikiwemo kifedha ili
itekeleze miradi hiyo kwa ufanisi na kwa wakati kutokana na umuhimu wa miradi hiyo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa, nchi ya Tanzania bado ina uhitaji wa umeme wa kutosha utakaotokana na vyanzo mbalimbali ikiwemo maji hivyo amekaribisha kampuni kutoka China kuja kuwekeza kwenye eneo hilo.
Dkt. Biteko amemweleza pia Balozi, Mingjian kuhusu mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ambapo ameeleza kuwa nchi ya Uganda na Tanzania zinauthamini mradi huo na zinaendelea na utekelezaji wake ambapo kampuni kutoka China ya CNOOC ni moja ya Wabia wa mradi huo.
Kwa upande wake, Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian naye ameeleza jinsi China inavyouthamini ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na China na kielelezo kikiwa ni ujio wa Rais wa nchi hiyo nchini Tanzania mwaka 2013 na mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Rais wa Tanzania, Dkt, Samia Suluhu Hassan na Rais wa China, Xi Jinping.
Kuhusu suala la kampuni za China kuja kuwekeza Tanzania kwenye miradi ya Nishati amesema kuwa, atazikaribisha kampuni hizo, huku akitolea mfano kampuni ya Synohydro ambayo inafanya vizuri ujenzi wa miradi ya uzalishaji umeme wa maji.