Featured Makala

TEKNOLOJIA MBADALA UJENZI WA BARABARA,MADARAJA YA MAWE ULIVYOMVUTIA WAZIRI MCHENGERWA

Written by mzalendo

  

Na.Catherine Sungura, Dodoma

Ni dhahiri kwamba mtandao imara na madhubuti wa barabara za mijini na vijijini una mchango mkubwa katika kukuza na kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja, familia jamii na Taifa kwa ujumla.

Ubunifu katika ujenzi wa barabara zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umemvutia mno Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa.

Hivi karibuni Waziri Mchengerwa aliitembelea TARURA kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Hakusita kuipongeza TARURA kwa kutumia teknolojia mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara ya mawe ‘cobble stone roads’ na madaraja ya mawe ‘stone arch bridges’.

Aidha, aliipongeza TARURA kwa kufanya majaribio ya teknolojia nyingine katika kuboresha barabara wanazosimamia.

Matumizi ya teknolojia na malighafi za ujenzi zinazopatikana eneo la kazi ikiwemo mawe katika  ujenzi na matengenezo ya barabara, huongeza ufanisi, huokoa muda, hutunza mazingira kwa gharama nafuu.

“Matumizi ya teknolojia mbadala na malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi kwa ajili ya ujenzi wa barabara na madaraka imeweza kupunguza gharama zaidi ya 50%.

“ ambapo TARURA imeweka kipaumbele cha kutumia malighafi  zinazopatikana maeneo ya kazi ili kupata ufanisi wa gharama za ujenzi,” anasema.

Takwimu za TARURA zinaeleza hadi kufikia mwezi Machi, 2023 imejenga madaraja 163 ya mawe yenye thamani ya Bilioni 8.7.

Gharama zimepungua na mikoa iliyojengwa  madaraja  hayo ni Kigoma(92), Singida (24), Tabora (5), Kilimanjaro  (10), Mbeya (2), Arusha (6), Morogoro (2), Rukwa (3), Pwani (1), Ruvuma (3) na Iringa (15).

Hata hivyo TARURA bado inaendelea kufanya majaribio ya teknolojia mbalimbali  ili kutumia udongo uliopo eneo la kazi  badala ya kusomba kutoka maeneo mengine mbali.

Katika ziara hiyo kwenye ofisi zake zilizopo Mji wa Serikali – Mtumba, Waziri Mchengerwa alizungumza na Menejimenti ya TARURA,  watumishi wote wa TARURA Makao Mkuu pamoja na watumishi wa TARURA Mkoa wa Dodoma.

Lengo la ziara hiyo ni kujadili  mambo muhimu kuhusiana na mipango ya utekelezaji wake  katika ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya barabara za Wilaya nchi nzima.

Barabara hizo ni zile ambazo TATURA inazisimamia kwa karibu kuhakikisha kwamba zinatoa huduma inayokusudiwa  kipindi chote cha mwaka.

MSINGI WA TARURA

TARURA ina jukumu la kusimamia matengenezo, ukarabati na ujenzi wa Barabara zenye urefu wa Kilomita 144,429.77.

Wakala huu pia una majukumu mengine kama yalivyoainishwa kwenye hati ya uanzishwaji wake ikiwamo kupima.

Aidha, kufanya utafiti kuhusu vifaa vya ujenzi kupitia Maabara Kuu ya Vifaa na Utafiti, kudhibiti uzito wa magari barabarani na kulinda maeneo ya hifadhi za barabara.

Waziri Mchengerwa aliipongeza TARURA kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya tangu kuanzishwa kwake.

Aliwahimiza waendeleee kuboresha utendaji wao katika kujenga barabara kwa viwango stahiki na kwa kuzingatia thamani ya fedha ili maendeleo ya kiuchumi na kijamii maeneo ya vijijini  na mijini yaendelee kukua.

Alisema tangu kuanzishwa kwa Wakala huyo mwaka 2017 kumekuwa na ongezeko la barabara za lami kutoka kilomita 1,449.55 hadi kilomita 3,053.26 sawa na ongezeko la 110%.

Pia, barabara za changarawe zimeongezeka kutoka kilomita 24,405.40 hadi kilomita 38,141.21 sawa na ongezeko lako la 56%.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeongeza fedha za matengenezo,ukarabati na ujenzi wa barabara na madaraja,

“..,  kutoka Tsh. Bilioni 275.03 mwaka 2020/21 hadi kufikia Tsh. Bilioni 836.237 kwa mwaka wa fedha 2021/22,2022/23 sawa na ongezeko la 204% na mwaka huu 2023/2024”. 

WAKANDARASI WA NDANI

 

Kwa upande mwingine, Waziri Mchengerwa aliitaka TARURA kulipa kipaumbele jukumu la kukuza na kuwaendeleza wakandarasi  wazawa ili kutoa mchango mkubwa kwa Taifa.

Aliitaka kuwataka kuyatambua makampuni ya wakandarasi 20 kila mkoa, hivyo alitangaza rasmi mkakati wa kukuza na kuendeleza wakandarasi wazawa.

Alisema hatua hiyo inalenga wafikie viwango vya kimataifa vya ubora na usalama na kuongeza kwamba Serikali imejipanga vyema kuhakikisha inawanyanyua wakandarasi wazawa. 

“Hatuwezi kuitenganisha TARURA na wakandarasi wa ndani kama ambavyo huwezi kuitenganisha TAMISEMI na wananchi.

“Maendeleo ya miundombinu yanamchango katika uchumi wa wananchi na wa Taifa,” alisisitiza.

Waziri Mchengerwa aliongeza “Mikakati ya TARURA ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 tuwe tumeboresha barabara za vijijini na mijini kwa asilimia 85.

“Lakini tukiwa tunaenda kuyafikia mafanikio hayo lazima tujiulize tumewakuza na kuwajenga wakandarasi wangapi wazawa tumewanyanyua kiasi gani kufikia viwango vya kuwafanya washindane kimataifa.”

“Kwa hiyo ninawataka, pamoja na majukumu mengi mliyonayo TARURA kwenye uongozi wangu kama Waziri jukumu la kukuza na kuwaendeleza wakandarasi wazawa nitalipa kipaumbele cha hali ya juu. 

Aliongeza “.., na leo natangaza rasmi mkakati wa kukuza wakandarasi wazawa utakaosimamiwa na ninyi   TARURA.

“Nitawapa TARURA mnisaidie ili tunakokwenda tuwe tumewajenga wakandarasi  angalau kila mkoa  kampuni za wakandarasi 20 tutakua kumekuza Kampuni za Wakandarasi takribani 520 katika mikoa yetu yote 26.

“Tukiyashika mkono kampuni ya wazawa wa Kitanzania 20 kila mkoa ina maana tutafungua uchumi na kustawi kwa kila mkoa, pia itawezesha kuimalisha kazi za wakandarasi hao kwa kila mkoa.”

Alisema mpango mkakati huo ni wa kuziwezesha kampuni za wazawa za ujenzi ili ziweze kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi inayotangazwa na TARURA.

“Lengo kuu la mpango huu ni kuboresha mazingira ambayo mjasiliamali wa Kitanzania wanaweza kufaulu, kukua na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi “.

KASI ZAIDI

Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff  alisema maagizo yote yaliyotolewa na Waziri wameyapokea na kuhakikisha watayafanyia kazi maagizo yote waliyopewa.

“Ikiwemo kusimamia kazi zote zinazotelelezwa ili ziwe na ubora za zenye matokeo yanayotarajiwa na wananchi,” alisema.

Kwa upande wa wa mameneja wa wilaya na mikoa, alisema wataendelea kutilia mkazo mahusiano mazuri ya kikazi ili kuepuka kuzorotesha kazi zinazoendelea.

“Hivyo wale wote watakaowaoana wanaweza kuwaleta shida au kuwakwamisha basi hawatosita kuwachukulia hatua.

“Kuhusu matumizi ya teknolojia mbadala Mhandisi Seff  alisema huo ndio muelekeo wa TARURA wa kupunguza gharama na kutunza mazingira ya nchi na hivyo wataendelea kulifanyia kazi zaidi.

Aliwasisitiza watumishi wenzake kuendelea kufanya kazi ili kuweza kutimiza malengo ya serikali kwa wakala huo.

Kwa upande wa kukuza wakandarasi wazawa, alisema watashirikiana na bodi ya wakandarasi nchini pamoja na taasisi za kifedha.

“.., na watakua mstari wa mbele kwa kuifanyia kazi kwa kuwainisha wakandarasi wale wanawataka ili waweze kutoka nje ya nchi kushindana na kuwa wa Kimataifa,” alibainisha.

About the author

mzalendo