Featured Kitaifa

WATU ZAIDI YA LAKI TATU KUPATA CHANJO DHIDI YA MATENDE NA MABUSHA KINONDONI

Written by mzalendo

Na WAF – Dar Es Salaam

Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTD) kwa kushirikiana na wadau wa Research Triangle Institute (RTI) inatarajia kufanya zoezi la umezeshaji kingatiba dhidi ya Ugonjwa wa Matende na Mabusha au Ngirimaji kuanzia Tarehe 6 mpaka 12 mwezi Disemba mwaka 2023 katika Manispaa ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaam kwa Wananchi Takriban 333,584 wenye umri wa kuanzia miaka mitano na kuendelea.

Akifungua mafunzo kwa Waandishi wa habari kuhusu Ugonjwa Wa Matende na Mabusha ili waweze kushiriki katika kuelimisha na kuhamasisha jamii iweze kushiriki kwenye zoezi la umezeshaji wa kingatiba hizo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule amesema Wilaya ya Kinondoni itahakikisha inaendelea kuweka jitihada za kutosha katika kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele (Mabusha na Matende).

“Ni wajibu wetu kuhakikisha tunaongeza uelewa kwenye masuala ya magonjwa yasiyokuwa hayapewi kipaumbele (NTD) lakini pia tunakuwa sehemu ya kutoa elimu na hamasa na kufuatilia katika ngazi za Jamii kila tunapopata nafasi ya kuzungumza na wananchi ili wawe sehemu ya kupata chanjo kama ambayo imeelekezwa”. Amesema Mhe. Mtambule .

Mhe. Mtambule amesema magonjwa haya yanaweza kuzuilika kwa kupata chanjo/kingatiba ama kupata tiba kwa ambao wanaugua na kwa kufanya hivyo tunaweza kuyaondoa kabisa kwenye jamii yetu.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Kinondoni Dkt. Samwel Laizer amesema kingatiba hizo zinatarajiwa kutolewa katika kata 10 za wilaya hiyo ambazo ni Kigogo, Mzimuni, Magomeni, Ndugumbi, Tandale, Kijitonyama, Kinondoni, Hananasif, Mwananyamala na Makumbusho kwa watu wote kuanzia miaka mitano na kuendelea.

“Tumepanga kugawa chanjo hii nyumba kwa nyumba katika jamii husika, na katika maeneo ya yote mikusanyiko ikiwemo Mashuleni, nyumba za ibada, Masoko, Stendi za Mabasi na Vituo vya kutolea huduma za Afya, katika kata husika lengo ni kuhakikisha kwamba walengwa wote wanapata dawa ili tuweze kuyatokomeza Magonjwa hayo”. Amesema.

“Tunagawa kingatiba hizi kwa sababu tukimeza wote katika jamii tunapunguza maambukizi kwa wakati wote na kuongeza kinga kwa wagonjwa pamoja na kupunguza ongezeko la ugonjwa wa matende na mabusha”. Amesema.

Nae Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Kinondoni Mhe. Songoro Mnyonge ametoa wito kwa watu wote wenye dalili za ugonjwa wa matende na mabusha wajitokeze kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya ili waweze kutibiwa maana magonjwa hayo yanatibika na kupona kabisa.

“Tumekuwa na imani nyingi huko nyuma kwamba magonjwa haya yanawapata tuu watu wa pwani lakini sasa hivi mtu yeyote anaweza akapata magonjwa haya, wagonjwa hawa walikua wanafichwa lakini sasahivi matende yanatibika na mabusha yanatibika katika vituo vyetu vya kutolea huduma za Afya”. Amesema.

About the author

mzalendo