Waziri wa habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nauye akizungumza katika kongamano la 7 la TEHAMA linalofanyika kwa siku 5 katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere JNICC jijini Dar es Salaam Leo Oktoba 16,2023.
Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nauye akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo Bw. Gerson Msigwa katikati na Mobhare Matinyi Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali katika kongamano la 7 la TEHAMA linalofanyika kwa siku 5 katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere JNICC jijini Dar es Salaam
………………………………
Waziri wa habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nauye amewataka wadau wa tehema kuwapa nafasi watu wa makundi maaluum katika maboresho ya teknolojia kwa kusikiliza maoni yao.
Hayo ameyasema leo Oktoba 18 jijini Dar es Salaam wakati akifungua kongamano la 7 la TEHAMA linalofanyika kwa siku 5 katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere JNICC.
Amesema kongamano hilo limezingatia ushiriki wa makundi yote ikiwemo vijana na wanawake.
“Nimeona kwenye majadiliano mmeweka siku maalumu kwa ajili ya wanawake na vijana hii ni nzuri kwani ripoti ya Dunia inaonyesha ushiriki wa wanawake kwenye TEHAMA ni mdogo basi kongamano lijalo muangalie namna ya kuwahusisha watu wenye makundi maalum wakiwemo walemavu”amesema.
Amesema serikali imeingia makubaliano na serikali ya India katika kuboresha Tehama hivyo wanapaswa kutumia fursa ya makubaliano hayo katika kujijengea uwezo na kupata uzoefu ili kuifanya nchi kuwa kitovu cha teknolojia bunifu.
Amesema mafanikio hayo yanalenga kufikia maono yalioonyeshwa kwenye mkakati wa uchumi wa kidigitali ambao umeandaliwa na wizara kwa kushirikiana na ofisi za umma na binafsi ambapo mkakati huo upo kwenye hatua za mwisho kupelekwa kwenye maamuzi.
Aidha Nape ameongeza kuwa kufanya ushirikiano na nchi zilizopiga hatua kutasaidia kuiwezesha nchi kusonga mbele kwenye matumizi ya teknolojia.
“Tunayo kila sababu ya kufanikiwa kwenye Tehama kwani mazingira tuliyonayo,miundombinu,utashi wa kisiasa uliopo,uwekezaji uliowekwa kwenye miundombinu hatuna sababu ya kubaki nyuma”amesema Nape.
Amesema matumizi ya teknolojia inayoibukia inawezeshwa pamoja na miundombinu rafiki ambapo serikali inatambua juhudi zinazofanywa na sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu hiyo ya mawasiliano.
“Hivi karibuni tumesaini leseni nne za Data Centers hii inaonyesha ni kwa jinsi gani wawekezaji wanaridhika na mazingira yaliyowekwa nchini katika kuhakikisha sekta ya Tehama inakua na ongezeko lake linaenda kugusa maisha ya watu”ameongeza
Amesema juhudi za makusudi zinapaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha hakuna anaeachwa na teknolojia hiyo ili kuleta uchumi jumuishi wa kidigital.
Amesema takwimu za watumiaji wa inteneti zimeongezeka kutoka milioni 29.9 mwezi Aprili 2022 hadi milioni 34.04 mwezi juni 2023 ambapo ni Sawa la ongezeko la asilimia 13.8.
“Mafanikio haya yanaenda sambamba na uhitaji wa wananchi kuelimishwa kuhusu usalama wa mitandao na namna gani wanaweza kujilinda kutumia mitandao hii kwa manufaa yao wenyewe”amesema.
“Matumizi ya Teknolojia zinazoibukia yanaenda sambamba na uhatarishi wa taarifa zetu binafsi hivyo jambo la msingi watumiaji wa huduma kufuata maelekezo ya wataalam”ameongeza.
Kwa upande wake mwakilishi wa kamati ya bunge ya miundombinu Livingstone Lusinde amesema bunge litaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa kwa kuchambua miswada mbalimbali ya kisheria itakayopelekwa bungeni lakini pia kupitisha ongezeko la bajeti kwa wizara hiyo.
Naye,Naibu waziri wizara ya Habari mawasiliano na teknolojia ya Habari Andrew Kundo amemshukuru Rais Dk.Samia kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki katika ukuaji wa sekta ya TEHEMA ndani ya nchi lakini pia kuvutia uwekezaji katika sekta hiyo.
Kongamano la 7 la TEHAMA ambalo litafanyika kwa muda siku tano linatumika kama jukwaa muhimu kwa wadau wote wa tehema kubadilishana mawazo uzoefu na kuibua fursa zilizopo hivyo linatarajiwa kutoka na maazimio ambayo yataishauri serikali namna bora ya kuwezesha sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa kidigitali ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema”Kutumia teknolojia ibukizi katika mapinduzi ya kidigitali ili kuzalisha ajira na kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii”