Featured Kitaifa

MUHIMBILI,JESHI LA POLISI NA RRH ZA DAR ES SALAAM WAKUTANA

Written by mzalendoeditor

Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo umekutana na Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Temeke, Amana, Mwananyamala, Waganga Wakuu wa Manispaa hizo, Kamishna Msaidizi wa Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi Jinai (Forensic Bureau), Msaidizi wa Kamishna Mkuu wa Upelelezi-Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Mganga Mkuu wa Mkoa huo ili kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo usimamizi wa vyumba vya kuhifadhi maiti.

Akifungua kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Mohamed Janabi amesema Hospitali ina majokofu 16 yenye uwezo wa kuhifadhi maiti 64 ambapo kila jokofu hubeba maiti nne ambapo kwa sasa inafanyiwa ukarabati mkubwa uliohusisha ununuzi wa majokofu mapya ya kisasa yenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya maiti 99.

Tayari majokofu saba yamewasili ambayo kila moja lina uwezo wa kubeba maiti sita sawa na jumla ya maiti 42. Majokofu mengine 11 zaidi yenye uwezo wa kuchukua maiti 57 yanatarajiwa kuwasili katikati ya mwezi wa Novemba mwaka huu.

Prof. Janabi amesema ni muhimu taasisi hizi kushirikiana katika suala la utunzaji wa maiti zile zinazohitaji uchunguzi wa sababu za kifo (medical legal postmortem) kulingana na eneo mwili huo ulipotokea ili kupunguza msongamano na kushirikiana katika kubeba gharama za uendeshaji.

Katika hatua nyingine Prof. Janabi amesema kuwa MNH iko tayari kutoa watalaamu kwenda kufanya uchunguzi katika maeneo husika na kuwajengea uwezo watalaam wa Hospitali hizo ili waweze kuendelea kufanya wenyewe.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Rashid Mfaume amesisitiza kuwa hakuna haja ya maiti kutoka sehemu mbalimbali za mkoa kupelekwa MNH kwani Hospitali mbalimbali za Rufaa za Mkoa huo na za Wilaya zina uwezo wa kuhifadhi maiti zisizopungua 85.

DKt. Mfaume amewataka Waganga Wakuu wa Hospitali Rufaa za Mkoa na Wilaya kushirikiana na MNH katika kuhakikisha huduma za kuhifadhi maiti na uchunguzi katika maeneo yao unaimarishwa kufuata viwango na ubora unaotakiwa.

About the author

mzalendoeditor