Featured Kitaifa

NDEJEMBI ATOA SIKU SABA MILANGO YA SHULE YA MSINGI TONYA IBADILISHWE

Written by mzalendoeditor

NA OR-TAMISEMI

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (0R-TAMISEMI), Mhe.Deogratius Ndejembi ametoa siku saba kwa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya kuhakikisha kuwa anasimamia milango iliyowekwa kwenye ujenzi wa Shule ya Msingi Tonya kubadilishwa ili kuendana na thamani ya fedha iliyotumika kwenye ujenzi huo.

Mhe.Ndejembi ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kukagua shule tatu za msingi zinazotekelezwa kupitia Mradi wa BOOST na shule mbili za sekondari zinazotekelezwa kupitia mradi wa maboresho wa SEQUIP katika Jiji la Mbeya.

Akiwa shuleni hapo Mhe.Ndejembi amesema, pamoja na kuona mradi wa shule hiyo mpya umekamilika, lakini hajaridhishwa na baadhi ya maeneo ikiwemo baadhi ya milango kuanza kupasuka mapema na hivyo kuagiza milango hiyo kubadilishwa haraka ndani ya siku saba.

“Nimefanya ziara kwenye shule tatu za msingi na mbili za sekondari, niwapongeze Jiji la Mbeya kwa kasi kubwa mliyonayo ya kutekeleza miradi hii iliyoletwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, haya mapungufu niliyoyaona niagize yafanyiwe kazi haraka na ndani ya siku saba yawe yamefanyika.

“Niziagize kamati zinazosimamia miradi hii nchi nzima kuhakikisha mafundi na wazabuni mnaowapa tenda hizi mnawasimamia katika kuhakikisha wanaleta vifaa vilivyo na ubora na ujenzi pia unatekelezwa kwa ubora ili kuendana na thamani ya fedha ambayo Rais wetu Dkt.Samia ameileta ili kuwahudumia watanzania.

“Niwaagize pia wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa wazabuni na mafundi ambao watashindwa kutekeleza miradi hii kwa ubora uliowekwa basi wachukuliwe hatua na wasiwape tenda nyingine na badala yake muwape kazi wazabuni na mafundi wenye kujali fedha hizi zinazoletwa kwa ajili ya maendeleo,”amesema Mhe.Ndejembi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, John Nchimbi amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi za miradi ya maendeleo zilizoletwa ndani ya jiji hilo ambapo ameahidi kuwa watashughulikia changamoto zote zilizobainika kwenye ziara ya Mhe.Naibu Waziri Ndejembi katika muda wa siku saba uliotolewa.

About the author

mzalendoeditor