Featured Kitaifa

BRAZIL YAJIPANGA KUANZA KUFUNDISHA KISWAHILI

Written by mzalendoeditor

Lugha ya Kiswahili ikiwa ni moja ya lugha zinazotambuliwa kimataifa na kupewa siku ya kuadhimishwa, Nchi mbalimbali zimeanza kufundisha lugha hiyo na nyingine kujipanga kuanza kuifundisha ikiwemo nchi ya Brazil.

Hayo yamedhihirika leo jijini Dodoma wakati Balozi wa Tanzania nchini Brazil Mhe. Prof. Balozi Adelardus Kilangi alipokutana na kuzungumza na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda kuhusu utekelezaji wa azma hiyo nchini humo.

Akizungumza katika kikao hicho Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Vyuo Vikuu vina nafasi ya kutoa wataalamu wanaoweza kwenda kufundisha huku wakijiendeleza kimasomo.

Baadhi ya Vyuo vilivyopendekezwa kuingia kwenye mpango wa mwanzo wa kufundisha lugha ya Kiswahili nchini huko kwa utaratibu wa makubaliano kati ya Vyuo vya Tanzania na Vyuo vya Brazil ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ( UDSM) Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na Chuo Kikuu kimoja cha Binafsi kitakachopendekezwa.

“Mhe Balozi tunaomba usaidie kupata udhamini wa masomo nchini humo watu wetu waje wasome mafunzo mbalimbali ikiwemo ukalimani na lugha, Sayansi, Teknolojia na uhandisi
huku wakiendelea kufundisha lugha ya Kiswahili “, amesema Prof. Mkenda

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Brazil Mhe. Balozi Prof. Adelardus Kilangi amesema amefika nchini na ujumbe wake akiwa na agenda mbalimbali ikiwemo kushirikiana na Wizara kuhakikisha lugha ya Kiswahili inafahamika nchini Brazil.

Amesema lugha ya Kiswahili inatambulika rasmi hivyo Balozi zetu zimepaswa kuikuza lugha hiyo akisema nchi nyingi zimeanza kufundisha.

Ametaja baadhi ya mipango waliyo nayo katika kuikuza lugha ya Kiswahili nchini humo kuwa ni kuhakikisha inafundishwa kwenye moja ya Chuo Kikuu kilichopo katika mji wa Brasilia nchini humo ambacho kinafundisha lugha za Afrika.

Aidha amesema wataanzisha darasa ubalozini ili kutoa fursa kwa watu wengi zaidi kuendelea kujifunza lugha hiyo pamoja na kuanzisha ” _Tanzania House”_itakayotangaza na kunadi utamaduni na bidhaa za Tanzania ikiwemo Kiswahili.

“Tayari tumepata fedha za kuanzisha Tanzania House katika mji wa SaoPaulo, tunataka kuona vitu vinavyotangaza utamaduni wa mtanzania vikiwekwa pale na kuendelea kuikuza pia lugha ya nchi yetu,”amesema Balozi Kilangi

About the author

mzalendoeditor