Featured Kitaifa

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAENDELEA KUWAJENGEA UWEZO VIONGOZI WA WMA KUSIMAMIA RASILIMALI ZA WANYAMAPORI

Written by mzalendoeditor
Na Mwandishi Wetu, IRINGA
Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuimarisha shughuli za uhifadhi nchini kwa kutoa mafunzo kwa Viongozi wa Jumuiya za Uhifadhi wa Wanyamapori (WMAs) za WAGA ( katika Wilaya ya Mufindi) na CHAMWINO (katika Wilaya ya Chamwino) lengo likiwa ni kujenga uelewa wa pamoja juu ya umuhimu wa kusimamia rasilimali za wanyamapori hasa katika maeneo ambayo wananchi wametenga maeneo yao kwa ajili ya uhifadhi.
 
Akizungumza leo mkoani humo, kwenye mafunzo ya viongozi wa WMA za WAGA na Chamwino kuhusu usimamizi na uendelezaji wa maeneo ya Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori, Mwakilishi wa Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori wa Wizara hiyo, Rose Mdendemi amesema wanatarajia baada ya mafunzo hayo viongozi hao watakuwa na nafasi nzuri za kuendeleza uhifadhi na kusimamia rasilimali katika maeneo ya Jumuiya hizo.
 
Bi. Mdendemi amesema mafunzo hayo yamewezeshwa kupitia Mradi wa Kudhibiti Ujangili na Biashara Haramu ya Nyara (IWT – PROJECT) unaotekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii ambao unalenga Wananchi wanashiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi nchini, kudhibiti ujangili, kupambana na wanyamapori wakali na Waharibifu na kuhakikisha wananchi wananufaika kupitia shughuli za utalii.
 
“Kwa kifupi tunaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan hasa katika kuendeleza utalii kwa kuwezesha wananchi kuwapatia ujuzi wa namna ya kusimamia maeneo yao ya hifadhi na kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyamapori wakali na wabaribifu” ,amesema.
 
 
“Tunawashukuru wenzetu wa UNDP wanatusaidia katika kutekeleza majukumu haya. Tunaamini kupitia mafunzo haya yatawezesha wananchi kusimamia rasilimali hizi vizuri na hatimaye kufikia malengo ya kuinua uchumi wa wananchi na taifa kwa Ujumla”, aliongeza Bi. Mdendemi
 
Kwa upande wake, Rachel John Afisa Wanyamapori Mkuu kutoka wilaya ya Mufindi Pamoja na Afisa Wanyamapori Mkuu wa Wilaya ya Chamwino mkoa wa Dodoma, Yusuph Nyonyi wameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwezesha kufanyika kwa mafunzo hayo ambayo ni muhimu katika jamii zilizotoa maeneo yao kwa ajili ya shughuli za uhifadhi
 
Naye Mwakilishi Kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Damas Masologo amesema nimatarajio ya Shirika hilo kuwa Mradi utapokuwa umekamilika, Jumuiya mbalimbali za Wanyamapori nchini zitakuwa zimesimama vizuri hasa katika kutekeleza majukumu yao.

About the author

mzalendoeditor