Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dkt.Alphonce Chandika ,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Agosti 1,2023 jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya hospitali hiyo na mwelekeo wake kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIKA mwaka wa Fedha 2023/24 Hospitali ya Benjamin Mkapa imetengewa Sh.Bilioni 64.52 ambapo kati ya hizo Sh. Bilioni 18.62 zinakwenda kwenye miradi ya maendeleo ili kuendelea kuwapunguzia wananchi adha ya kusafiri mbali kupata matibabu.
Hayo yamesemwa leo Agosti 1,2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk.Alphonce Chandika wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya hospitali hiyo na mwelekeo wake kwa mwaka wa fedha 2023/24.
“Maendeleo hayo ni kuendeleza ujenzi wa jengo la saratani ambao mpaka sasa umefikia asilimia 27, hivyo kwa kutengewa fedha hizi zitasogeza zaidi ujenzi, eneo lingine ni ujenzi wa jengo la matibabu ya moyo na kifua kwa watoto na watu wa zima tunatarajia kuanza ujenzi huu mwaka huu wa fedha nayo ni katika lengo la kuwapunguzia adha wananchi kusafiri mbali kupata matibabu,”amesema Dkt.Chandika
Aidha amesema kuwa bajeti hiyo inakwenda kuwezesha kujenga kituo cha upandikizaji wa figo yenye vyumba vya upasuajia kwa anayechangia figo na anayepokea.
Hata hivyo Dkt.Chandika ameweka wazi mafanikio ya huduma za kibingwa yaliyopatikana ikiwamo upandikizaji wa uume ambao unagharimu sh.milioni sita hadi 10.
Amesema kuwa huduma hiyo iliyofanywa kwa wanaume wawili waliokuwa na tatizo la nguvu imeonesha matokeo mazuri na kurejesha heshima kwa familia zao.
“Tumeona hata wenzetu waganga wa kienyeji wanapita huko mtaani kule na dawa ya kutibu tatizo hili, wananchi wanasumbuka sisi kama taasisi ya umma tuje na mkakati wa kuwasaidia wananchi, tulianza kutoa huduma mwezi Juni 2022 kwa kuhudumia wanaume wawili lakini kwa habari njema kutoka kwao mambo ni mzuri.”
“Mambo ni mzuri sana kwasababu tuliwapa masharti wakae wiki sita ndio waanze kujaribu mitambo, mitambo imekaa vizuri na wao wametuambia matokeo mazuri wamefurahi sana na imerejesha heshima kwenye familia zao,”amesema
Hata hivyo,Dkt.Chandika amesema wapo kwenye mchakato wa kuongeza wigo wa utoaji huduma ili zipatikane kwa wahitaji wote na wale wanaotengeneza vipandikizi wanakamilisha taratibu za usajili ili kufungua ofisi Dar es salaam itakayorahisha upatikanaji wake.
“Natumaini baada ya kuanza sisi na hospitali zingine zitatoa kwa kuwa uhitaji ni mkubwa sisi pekee yetu hatutatosheleza, kwa hiyo tutashirikiana na wenzetu hata kuwapa mafunzo ili watoe huduma kwenye hospitali zao,”amesema
Hospital ya Benjamin Mkapa inahudumia wananchi zaidi ya Milioni 10 wa mikoa ya Dodoma,Iringa,Singida,Manyara na baadhi ya maeneo ya mikoa ya Morogoro na Tabora pia inapokea Wananchi kutoka karibu Kila Kona ya Nchi na nje ya mipaka ya Tanzania wanaokuja kufuata huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi.