Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule (wa kwanza kushoto) akimsikiliza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino (hayupo pichani) katika kikao cha Baraza la Madiwani kikao kilichojadili hoja za ukaguzi kwa Wilaya ya Chamwino. Wengine katika picha ni Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Gift Msuya na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akitetea jambo na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Gift Msuya katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Chamwino. Kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chamwino Edson Sweti na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Dkt. Semistatus Mashimba akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani kikao kilichojadili hoja za ukaguzi kwa Wilaya ya Chamwino. Wengine katika picha ni wajumbe wa Baraza la Madiwani Wilaya cha Chamwino.
Mwenyekiti wa Halmashauri Wilaya ya Chamwino akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani kikao kilichojadili hoja za ukaguzi kwa Wilaya ya Chamwino. Wengine katika picha ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Dkt. Semistatus Mashimba, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Gift Msuya
Sehemu ya wajumbe wa Baraza la Madiwani kutoka Chamwino walioshiriki katika kikao hicho kilichojadili hoja za ukaguzi kwa Wilaya ya Chamwino.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Madiwani mara baada ya kukamilika kwa kikao kilichofanyika hivi karibuni katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino.
Na.Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ametaka hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa watumishi wote ambao wamebainika kuhusika na vitendo vya ubadhirifu wa rasilimali au fedha za umma na kusababisha hoja za ukaguzi kwa uzembe.
Akizungumza katika Kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Senyamule amekemea vikali tabia ya baadhi ya watumishi kutotimiza majukumu na wajibu wao wa msingi kwa makusudi hali inayopelekea kukithiri kwa hoja za ukaguzi zisizokuwa na majibu.
“Kila mmoja atimize wajibu wake, hoja nyingi hapa zinatokana na uzembe wa baadhi ya watumishi kutotimiza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria, wanashindwa kuambatisha nyaraka za msingi zinazohitajika hali inayopelekea kukithiri wa hoja za ukaguzi. Senyamule ameonya.
Amesema ili Halmashauri hiyo kuondokana na hoja nyingi ni lazima Kamati ya Fedha kukutana kila mwezi na kuwa na agenda ya kudumu ya kujadili mwenendo wa namna ya kujibu hoja za Mkaguzi wa ndani na zile za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kuchukua hatua stahiki pale inapobainika uzembe wa aina yoyote.
Senyamule pia, ametoa rai kwa madiwani hao kuhakikisha kuwa fedha zinapelekwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kuzingatia mgawanyo wa asilimia 40 na asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa mujibu wa Sheria. Pia amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chamwino Dkt. Semistatus Mashimba kuhakikisha mapato ya Serikali yanakusanywa kikamilifu na kudhibiti upotevu.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mapendekezo ya mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwa Halmashauri ya Chamwino, Bw. Chambi Ngelela Mkaguzi Mkuu wa Nje amesema Halmashauri hiyo ilipata hati inayoridhisha.
“Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ilikuwa na hoja 61 ambapo hoja 13 zimeweza kufungwa na kusalia na hoja 48 ambazo utekelezaji wake unaendelea.” Amesema Bw. Ngelela.
Aidha Senyamule katika hatua nyingine amewataka Viongozi hao wa ngazi ya Wilaya kuendelea kutunza Mazingira na kuanza maandalizi ya kuoteshea vitalu vya miche ya miti kwa ajili ya kupanda wakati wa msimu wa mvua unapokaribia ili kuwe na miche ya kutosha kwa kila Halmashauri kupanda miti milioni moja na laki tano kwa mwaka kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali.
“Katika kuendelea kukijanisha Mkoa wetu na kutunza Mazingira tuanze mapema maandalizi ya kuandaa vitalu vya miche na kila wilaya iwe na Miche ya kutosha isiyopungua milioni moja na laki tano. Hapa nisisitize kuwa katika kila wilaya nitakayofanya ziara kuanzia mwezi wa nane nitakagua vitalu hivyo vilevile hakikisheni mnatenga maeneo kwa ajili ya kunufaika na biashara ya hewa Ukaa na kila Wilaya angalau iwe na maeneo matatu kama tulivyokubaliana hapo awali”. Amesisitiza Senyamule