Featured Kitaifa

TOASTMASTERS INTERNATIONAL KUFANYA MKUTANO JIJINI DAR, WATU 200 AFRIKA MASHIRIKI KUHUDHURIA

Written by mzalendoeditor


Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

KIONGOZI wa Shirika lisilo la kiserikali Kanda ya Afrika Mashariki TOASTMASTERS INTERNATIONAL Emilia Siwingwa amesema kwamba watu zaidi ya 200 wanatarajia kushiriki kwenye mkutano wa mwaka wa shirikisho hilo unaotarajia kuanzia kesho Mei 19 jijini Dar es Salaam.

Siwingwa amesema kutokana na ukubwa wa mkutano huo pia wanachama wa ToastMasters International kutoka nchi sita za Afrika Mashariki ambao ni wanachama watashiriki na mgeni rasmi atakuwa Rais wa Shirika hilo Matt Kinsey ambaye makazi yake ni nchini Marekani.

Akizungumza jijini Dar Mei 18, 2023 jijini Dar es Salaam Siwingwa amesema shirika hilo lisilo la kiserikali limeundwa mwaka 1924, hivyo lina miaka takribani 99 na limekuwa likishughulika na masjala ya mafunzo ya mawasiliano ya uongozi lakini pia kumuwezesha mtu kuwa mwenye uwezo wa kufanya kazi na kuleta matokeo chanya kwenye jamii.

“Katika Afrika Mashariki ToastMasters International imeanza rasmi miaka sita iliyopita na nimeitambulika miaka mitatu iliyopita na iko katika nchi za Burundi, Ethiopia, Kenya Rwanda , Uganda pamoja na Tanzania, tuna wanachama 1600.

“Leo tumekutana hapa kutangaza tutakuwa na kikao cha mwaka na mwaka huu tumepata ugeni wa kipekee tumepokea Rais wa ToastMasters International na yeye ndio atatoa hotuba ya kuanzisha kikao chote siku ya Jumamosi asubuhi.

“Na tumealika ToastMasters kutoka Afrika Mashariki, hivyo tutakuwa na watu 200 watakaohudhuria ,wamekuja hapa , pia kutakuwa na watu ambao watahudhuria kwa kutumia njia mitandao mbalimbali,amesema Siwingwa.

Ameongeza wataanza rasmi kesho Ijumaa ambapo kutakuwa na hafla iliyoambatana na vinywaji katika hoteli ya Sea Cliff na Jumapili watakuwa Johari Rotana hoteli ambapo watamaliza kwa hafla hiyo kwa kutoa tuzo na hotuba mbalimbali kwa washiriki.

Pia amesema kesho watakuwa na hafla nyingine ambayo wamealika viongozi wa sekta binafsi, viongozi wa sekta isiyo ya kiserikali na baadhi ya watu kutoka serikalini kwa ajili ya kuzungumzia masuala hayo ya mawasiliano, uongozi pamoja na kuangalia fursa kwenye sekta ya biashara na uwekezaji nchini Tanzania.

“Kama tunavyojua sasa hivi tunaangalia masuala ya kuifungua Tanzania ili tuweze kunyanyua uchumi wetu na tumeona shughuli tunazofanya tunaendana sambamba na ajenda hizo sio tu katika Afrika Mashariki bali na duniani kote,”amesema.

Ametumia nafasi hiyo kuelezea pia ToastMasters iko katika nchi 149 na tuna wanachama zaidi 300,000 katika makundi mbalimbali na hadi sasa watu milioni sita wamefikiwa na shirika letu kupitia program mbalimbali.

“Kwetu sisi kuandaa mkutano huu ni jambo kubwa na la kipekee kwani ndio kwa mara ya kwanza mkutano unafanyika Afrika Mashariki na hasa Tanzania.Tiketi kwa ajili ya kushiriki mkutano huo wa siku tatu ni Dola 100 , hivyo tunawaalika watu mbalimbali kushiriki.”

Kuhusu uwekezaji , ameeleza katika sekta ya biashara na mfumo wa uwekezaji katika nchi yoyote ile duniani lazima kutakuwa na watu watakaowezesha malengo yaliyopangwa yafikiwe na hivyo wao wameona haja ya kusaidia watu kwa kutoa mafunzo ya kuboresha masuala ya mawasiliano na uongozi.

Pia wamekuwa wakiangalia maadili kwani wanaamini kwamba kiongozi mzuri ni yule ambaye atazingatia maadili na atachukia rushwa huku akifafanua katika taasisi au jamii jwatu wakiweza kufanya kazi kwa pamoja watafika mbali zaidi.

Ameongeza katika mawasiliano wanaamini sio tu kuwa na uwezo wa kuzungumza hapana bali wewe ni msikivu. Wengine wakiongea unawaelewa na utakachowajibu kitaendana na utakachosema.Pia wanaangalia jinsi gani wanaweza kuzungumza ili yule anayesikiliza anaelewa na ataguswa kiasi gani.

KIONGOZI wa Shirika lisilo la kiserikali Kanda ya Afrika Mashariki TOASTMASTERS INTERNATIONAL, Emilia Siwingwa (katikati)  akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu kufanyika kwa mkutano wa mwaka utakaofanyika jijini Dar es Salaam,Siwinga amesema watu zaidi ya 200 wanatarajia kushiriki mkutano huo wa mwaka wa shirikisho hilo unaotarajia kuanza leo Mei 19 jijini Dar es Salaam,pichani kulia ni Rais wa Shirika hilo , Matt Kinsey akifuatilia.

Rais wa Shirika  lisilo la kiserikali TOASTMASTERS INTERNATIONAL  Matt Kinsey akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani) namna shirika hilo  lenye Wanachama  wapatao 1600 kutoka nchi za Burundi, Ethiopia, Kenya Rwanda , Uganda pamoja na Tanzania walivyojiandaa kuhakikisha mkutano huo wa mwaka unafanikiwa kwa kiasi kikubwa.

KIONGOZI wa Shirika lisilo la kiserikali Kanda ya Afrika Mashariki ToastMasters International, Emilia Siwingwa akionesha nchi za Burundi, Ethiopia, Kenya Rwanda , Uganda pamoja na Tanzania ambazo zitashiriki mkutao huo wa Mwaka leo jijini Dar,ambapo mkutano huo utafunguliwa na Rais wa Shirika hilo Matt Kinsey.

About the author

mzalendoeditor