Featured Kitaifa

WARATIBU HUDUMA NDOGO ZA FEDHA WAPIGWA MSASA

Written by mzalendoeditor

Kamishna Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha, Bi. Dionisia Mjema akifafanua jambo wakati wa mafunzo ya waratibu wa biashara ya huduma ndogo za fedha yaliyofanyika jijini Dodoma.

Kamishna Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha, Bi. Dionisia Mjema, Afisa Mkuu Mwandamizi Idara ya Usimamizi wa Huduma ndogo za Fedha, kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Deogratias Mnyamani na Mwanasheria wa Serikali kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Bi. Antelma Mtemahanji, wakiteta jambo wakati wa mafunzo ya waratibu wa biashara ya huduma ndogo za fedha yaliyofanyika jijini Dodoma.

Afisa Mkuu Mwandamizi Idara ya Usimamizi wa Huduma ndogo za Fedha, kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Deogratias Mnyamani akitoa mada kuhusu taarifa ya utekelezaji wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 katika mafunzo ya waratibu wa biashara ya huduma ndogo za fedha yaliyofanyika jijini Dodoma.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya waratibu wa biashara ya huduma ndogo za fedha wakifuatilia kwa makini mada mbalimbali zilitolewa katika mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dodoma.

Mwanasheria wa Serikali kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Bi. Antelma Mtemahanji akitoa mada kuhusu Kanuni za Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha kwa vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha katika mafunzo ya waratibu wa biashara ya huduma ndogo za fedha yaliyofanyika jijini Dodoma.

Mchumi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Farida Makao akielezea Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha kuhusu majuku ya Waziri wa Fedha kwa waratibu wa biashara ya huduma ndogo za fedha katika mafunzo yaliyofanyika jijini Dodoma.

Meza kuu iliongozwa na Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya waratibu wa biashara ya huduma ndogo za fedha walio shiriki mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyofanyika jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango, Dodoma)

Na Farida Ramadhani, WFM-Dodoma.

Serikali imeandaa mafunzo ya waratibu wa biashara ya huduma ndogo za fedha ili kuwajengea uwezo na kupata mrejesho wa utekelezaji wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 na Kanuni zake za mwaka 2019.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo jijini Dodoma, Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamwaja, alisema mafunzo hayo ni mwendelezo wa mkakati wa Serikali kuwajengea uwezo waratibu pamoja na kujadili changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa Sheria na Kanuni hizo na mapendekezo ya kukabiliana nazo.

‘’Hii itasaidia pamoja na mambo mengine, kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya waratibu ya uhamasishaji wa sekta hii, usajili wa wahamasishaji wa biashara ya huduma ndogo za fedha na kukuza sekta hii muhimu nchini’’, alisema Dkt. Mwamwaja.

Alisema Sekta Ndogo ya Fedha imepitia changamoto nyingi ambazo zimesababisha Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2000 na kuandaa Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2017.

“Katika kutekeleza Sera hiyo, Serikali ilitunga Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 na Kanuni zake za mwaka 2019 ili kuweka mazingira wezeshi ya usimamizi na uendelezaji wa Huduma Ndogo za Fedha nchini kwa lengo la kuondoa changamoto katika sekta hii na kuongeza mchango wake katika kukuza uchumi na kuondoa umaskini”, alisema Dkt. Mwamwaja.

Aidha, aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa chachu ya kukuza maendeleo ya biashara ya huduma ndogo za fedha kwa kuwaelimisha wadau mbalimbali na kuwaelekeza fursa zilizopo katika biashara hiyo.

Kwa upande wake Afisa Mkuu Mwandamizi Idara ya Usimamizi wa Huduma ndogo za Fedha, kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Deogratias Mnyamani, ambao ndio wasimamzi wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha na Kanuni zake, alisema utekelezaji wa sheria hiyo na kanuni zake umeiwezesha Serikali kupata takwimu za watoa hudima na watumiaji wa Huduma Ndogo za Fedha.

Alisema mpaka kufikia Februari 2023, Benki ilipokea maombi 1,651 kwa daraja la pili, maombi 1,179 kwa kwa daraja la tatu na maombi 39,384 kwa daraja la nne ambapo kati ya maombi hayo, Benki Kuu imetoa leseni 1,158 kwa daraja la pili na leseni 773 kwa daraja la tatu.

Bw. Mnyamani alisema Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari kwa kuwa imebaini kuwa bado kuna changamoto ya uelewa wa sheria na kanuni zake kwa watoa huduma na watumiaji wa Huduma Ndogo za Fedha.

Nao baadhi ya washiriki wa mfunzo hayo wameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuendelea kutoa mafunzo hayo yatakayosaidia ukuaji wa Sekta ya Fedha na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Wameiomba Serikali ihakikishe elimu ya fedha inakuwa ajenda ya kudumu katika vikao kuanzia ngazi ya vijiji na kata.

Mratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Bw. Lodrick Mwakisole ni miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo ambaye amesema kuwa mafunzo hayo yataongeza nguvu na hamasa katika kutekeleza majukumu yao ya kusimamia na kuhamasisha biashara ya huduma ndogo za fedha katika jamii.

Naye Mratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Bi. Happiness Joachim, alisema ni vema Serikali ikaongeza uzito katika suala la usimamizi wa biashara ya huduma ndogo za fedha hasa katika masuala ya kibajeti na utoaji wa elimu.

Alipendekeza elimu itolewe zaidi kwa watumiaji wa huduma hizo kwa kuwa wao ndio wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo kudhurumiwa kutokana na kutokuelewa haki zao za msingi na kubaini vipengele tata vya masharti ya mikopo wakati wanakopa.

About the author

mzalendoeditor