Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amevitaka vyombo vya habari nchini kuwa wazalendo kwa kulinda amani, umoja na mshikamano wa kimataifa wakati vinatekekelza majukumu yake ya habari.
Ametoa wito huo hivi karibuni Visiwani Zanzibar wakati akihutubia katika maadhimisho ya sherehe za miaka 30 ya Siku ya Uhuru wa Vyombo Duniani, ambapo amesema kuwa Serikali zote mbili zimeendelea kuboresha mazingira ya sekta ya habari nchini na hivyo vyombo vya habari navyo vitekeleze majukumu yake kwa kuzingatia uzalendo na maadili ya taaluma ya habari.
“Ni matarajio yetu vyombo vya habari vinasaidia katika kulinda amani, umoja na mshikamano kimataifa pamoja na kutangaza raslimali za nchi yetu sambamba na kutoa taarifa chanya” Alisema Rais Dkt. Mwinyi.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewapongeza waandishi wa habari kutoka bara na visiwani kwa mchango wao kwa taifa na kuwataka kuendelea kuwa wazalendo kwa nchi yao.
“Lazima tutambue kuwa hakuna uhuru usio kuwa na mipaka wala uhuru usiokuwa na wajibu”. Alisisitiza Rais Mwinyi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi, Kundo Mathew alimpongeza Rais wa Zanzibar kwa kuwa katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake idadi ya vyombo vya habari vilivyosajiliwa Zanzibar imeongezeka.
Aliongeza kuwa Serikali zote mbili zimeendelea kufanya maboresho ya sheria zinazihusika na masuala ya habari huku akiahidi Serikali kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuharakisha maendeleo nchini.