Featured Kitaifa

WAZIRI JAFO ATANGAZA KUSITISHA MATUMIZI YA KUNI NA MKAA KWA TAASISI ZA UMMA NA BINAFSI

Written by mzalendoeditor

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais,(Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo,akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 12,2023 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu katazo la kusitisha matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi za umma,binafsi ifikapo Januari 31,mwakani. 

Na.Alex Sonna-DODOMA

SERIKALI kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imetangaza kusitisha matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi za umma na binafsi za Tanzania Bara zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 100 kwa siku ifikapo Januari 31 mwaka 2024.

Aidha kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya mia tatu wanatakiwa kusitisha matumizi hayo ifikapo Januari 2025.

Katazo hilo limetolewa leo Aprili 12,2023 jijini Dodoma Waziri wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais,(Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo, amesema katazo hilo amelitoa kwa Mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 13 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura ya 191

“Kwa Mamlaka niliyopewa chini ya Kifungu cha 13 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura ya 191, natoa katazo kwa taasisi zote za umma na binafsi zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 100 kwa siku kusitisha matumizi ya kuni na mkaa ifikapo Januari 31 mwaka 2024.”amesema Dkt.Jafo

Aidha amesema kuwa Taasisi zinazoandaa Chakula cha watu zaidi ya 300 kwa siku kusitisha matumizi hayo ifikapo Januari 31 mwaka 2025 badala yake taasisi hizo ziwe zinatumia nishati mbadala ambayo ni safi kwa ajili ya kupikia.

”Serikali imeweka nia ya kupunguza athari hizo ambapo imeandaa Dira ya Taifa ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia pamoja na Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Dira hiyo kwa kipindi cha miaka kumi hadi kufikia 2033.”amesisitiza Waziri Jafo

Hata hivyo Dkt. Jafo amesema kipaumbele cha serikali kwa sasa ni kujenga uchumi wa viwanda hivyo matumizi ya nishati mbadala yatatoa fursa ya viwanda vya kutengeneza mkaa mbadala .

Katazo hilo linafuatia baada ya Ripoti ya tatu ya hali ya Mazingira nchini ya mwaka 2019 kuonyesha kuwa kasi ya uharibifu wa misitu ni kubwa na kila mwaka zaidi ya hekta 469,420 huharibiwa kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa.

About the author

mzalendoeditor