Featured Kitaifa

ASKOFU KINYAIYA AKEMEA USHOGA NA USAGAJI,ATAKA KUNDI LA WATOTO,WANAWAKE NA WALEMAVU LIPEWE HAKI KATIKA JAMII

Written by mzalendoeditor

Na Ndahani Lugunya,Dodoma.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Mhashamu Beatus Michael Kinyaiya,ameonya na kukemea baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali yanayopigia debe vitendo vya ushoga na usagaji.

Ametoa onyo hilo wakati akitoa homilia yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu Dominika ya Pasaka, katika Kigango cha Mt.Peter Claver-Mlimwa “C” Parokia ya Mt.Inyasi wa Loyola-Miyuji Kusini Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.

“Kuna mashirika Ulaya kule na marekani ambayo yanamwaga Pesa nyingi sana kwetu sisi Waafrika ili tuanzishe Mashirika  yasiyo ya kiserikali na lengo ni kuwafanya vijana wapende ushoga na usagaji.

Na hata Dodoma nimesikia kipo kikundi na Tanzania yote hii hivi vikundi vimeenea na wanakazana sana hao watu kupigia kelele kwenye runinga na kwenye mitandao.halafu walivyo wajanja sasa unajua wenzetu wakiwa na jambo lao huwa wanaliweka hatua kwa hatua.

Hatua ya kwanza huwa wanaanza kwa kulidokeza,wanalidokeza kidogo.mkishaliona mnapiga kelele kwamba sisi hatutaki wanasema sawasawa  wanatulia.kwa mfano sasa hivi tunalipigia kelele wametulia.

Baada ya hapo wanaliibua tena na wanajua wanapoliibua mara ya pili mmeshalizoeazoea mtakubali na wamekuwa katika kuzungumza ndio wanatumia ujanja wao wote na ushawishi wao wote na kutumia watu maarufu kuling’ang’ania likubalike na baada ya kukubali mazungumzo baada ya muda utaona mmoja mmoja anaanza kujitoa na ndipo wanafanikiwa,” amesema.

Kutokana na kuenea kwa kasi vitendo hivyo Askofu Mkuu Kinyaiya amewataka Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema kutokukubali vitendo hivyo alivyo viita vya kishetani.

Katika kuendeleza mapambano dhidi ya vitendo hivyo vya ndoa za jinsia moja,amempongeza Rais wa Uganga Mhe.Yoweri Mseveni kwa kulisimamia kidete na kukataa kwa nguvu zote kuruhusu ushoga na usagaji katika taifa hilo.

“Nampongeza sana Rais wa Uganda amelisimamia kikamilifu na amesema hapana.nampongeza sana Rais wetu Mama Samia na yeye alisema tabia za watu wengine zisipandikizwe kwetu.kwa hiyo Serikali ya Tanzania nayo iko vizuri,” amesema Askofu Kinyaiya.

Amewaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuunga mkono jitihada za Viongozi wa Serikali katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo viovu,ambavyo kimsinmgi vinakwenda kinyume na amri za Mungu,Kanisa na tamaduni za Kiafrika.

“Sasa tunasaidia na sisi?  Viongozi kusema haitoshi watendaji tunaokutana na hivi vitu ni sisi wazazi marafiki.hivi vitu  wanaofanya ni marafiki zetu.kwa hiyo naomba wote tupaze sauti tusikubali kuingizwa katika hilo ni ushetani na hauna nafasi katika jumuiya hii ya Mwenyezi Mungu,” amesisitiza Askofu Kinyaiya.

Pamoja na sauala zima la ushoga na usagaji, Askofu Mkuu Kinyaiya amewataka waamini na  jamii yote kwa ujumla kulinda haki za watoto inavyotakiwa.

Amesema watoto kwa sasa wanapitia magumu na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ukatili wa kingono unaotokana na Imani za kishirikina,kwani wapo baadhi ya watu wa karibu wa watoto hao wanadanganywa na waganga wa kienyeji kwenda kuwafanyia ukatili watoto.

“Kuna watu ambao kwasababu sijui akili zao zimepinda au kwasababu ya ushirikina na kudanganywa na waganga wa kienyeji wanafanya vitendo vya aibu sana kwa watoto.na watoto wengi wanashindwa kuwaambia wewe mama au baba kwasababu huna muda wa kuongea nae walau kwa dakika chache tu.

Akitaka kuongea na wewe unamfukuza toka hapa unanisumbua,hapana naomba msikilize mtoto.na ninyi watoto mkiona jambo lolote haliendi vizuri kaa na mama umueleze ukiona mama hakusikilizi nenda kwa sisita,sista hakusikilizi njoo kwa Padri mueleze kwamba kuna hili na hili nafanyiwa mimi silipendi.kwa hiyo naomba sana tulinde haki za watoto” amesisitiza Askofu Kinyaiya.

Aidha pamoja na kulinda haki za watoto,amewataka waamini na jamii yote kulitazama kundi la akina mama kwa namna ya pekee,kwani wapo akina Mama wananyanyaswa na waume zao na kunyimwa haki zao msingi.

“Wanaume naomba sana tuwape akina mama heshima yao please (tafadhari).Yesu alipozaliwa kwa wayahudi wayahudi walikuwa wakiwaona akina mama sio watu sawasawa.na ndiyo maana leo katika Injili akina Mama wanapokwenda kusema Yesu amefufuka  watu hawakuamini .walisema akina mama hawa maneno mengi watakuwa wametudanganya wanakwenda kaburini kuhakikisha wenyewe.

Naomba tuwe na tabia ya kuwaheshimu akina Mama na kuwapa haki zao please (tafadhari) naomba sana.na wale wanaume ambao hawataki wake zao wafanye kazi au biashara eti kwasababu atakuwa na hela ili awe na kiburi hiyo tabia ni mbaya na ni unyanyasaji wa kijinsia,” amesema Askofu Kinyaiya.

Pamoja na makundi hayo,Askofu Mkuu Kinyaiya ameitaka pia jamii kulinda haki za walemavu,kwani wapo wanao nyanyapaliwa na wengine kufichwa katika kaya ili wasionekane katika jamii kwa dhana hasi ya kuficha aibu katika familia.

“Kundi la tatu ni walemavu.kuna familia zina walemavu lakini zinawaficha hawataki aonekane wanaona kama aibu sijui.Mungu alipenda iwe hivyo kwanini umfiche?.hutaki aende Shuleni hutaki afanye kazi zilizo ndani ya uwezo wake.tafadhari sana naomba sana wote tupaze sauti kusaidia hawa ambao wananyanyaswa,” amesema Askofu Kinyaiya.

Amehitimisha homilia yake kwa kuwatahadharisha Vijana waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda,juu ya uendeshaji wa pikipiki kwa mwendokasi jambo linalotokana na majivuno,matokeo yake wameendelea kuleta madhara barabarani ikiwa ni pamoja na kusababisha vifo na ulemavu wa kudumu.

“Naomba niongee na Vijana hivi mnaponunua bodaboda zenu akili huwa zinapinda? Mnaendesha pikipiki zenu kwa majivuno na kujionyesha matokeo yake mnatugonga mnagonga watoto akina Mama.kwanini msitembee kwa polepole kwa heshima na mfuate sheria za barabarani hayo majivuo ni ya nini?.

Mwishoni mnaumia mnavunjika miguu mnalalamika kwamba Mungu hatupendi,naomba sana tufaute sheria za barabarani na kuendesha kwa ustaarabu.tabia nyingine mbaya ni wivu mwenzako akipata kitu kizuri basi kiroho kisikuume ukamletea mtu wivu makusudi mazima ili umsumbue asipate maendeleo.muombee mwenzako aendelee na wewe kazana kufanyakazi utafanikiwa,” amesema Askofu Kinyaiya.

About the author

mzalendoeditor