Featured Kitaifa

TAA INATHAMINI MICHEZO KWA WATUMISHI-DG MBURA

Written by mzalendoeditor

Katibu Mkuu wa Klabu ya Michezo ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Bw. Mbura Tenga (kulia), akimkabidhi kombe la ushindi wa jumla , Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege Tanzania (TAA) walilolipata kutoka kwenye michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), pia michezo ya Mei Mosi na mabonanza.

 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege Tanzania, Bw. Mussa Mbura (wa kwanza kushoto) akimsikiliza Katibu Mkuu wa Klabu ya Michezo ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Utamaduni), Bw. Mbura Tenga (kulia), akitoa historia fupi ya klabu hiyo, kwenye hafla ya kukabidhiwa vikombe vya ushindi wa michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za serikali (SHIMIWI), Mei Mosi na mabonanza.

 

Baadhi ya wanamichezo wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Bw. Mussa Mbura (watano kutoka kulia), baada ya kukabidhi vikombe vya ushindi wa michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), Michezo ya Mei Mosi na bonanza.
****

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imesema inathamini michezo mahala pa kazi na itaendelea kuwaruhusu watumishi wake kushiriki kwenye michezo mbalimbali inayoandaliwa na mashirikisho yanayotambuliwa.
 

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Bw. Mussa Mbura alipokuwa akipokea vikombe zaidi ya 10 vya ushindi wa michezo ya mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI),  michezo ya Mei Mosi iliyofanyika mwaka 2022 mkoani Morogoro na Dodoma na bonanza lililofanyika kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
 
Bw. Mbura amesema TAA inathamini michezo kwa kuwa inawaweka watumishi wake katika afya njema ya mwili na akili, ambapo husaidia huongeza ufanisi wa majukumu yao ya kazi.
 
“TAA tunaahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa kuendelea kutoa wachezaji wengi kama sasa wanaounda timu yetu ya Sekta ya Uchukuzi, inayoshiriki kwenye michezo mbalimbali, sote tunajua michezo ni afya, upendo na inajenga mahusiano na watu wengine na inajenga afya ya mwili na akili vinakaa vizuri, kwa hiyo muendelee kushiriki na msiache kutimiza majukumu yenu,” amesema Bw. Mbura.
 
Pia amesema pamoja na klabu hiyo kuwa na kupewa kipaumbele na menejimenti yote, bado TAA wamepokea maelekezo ya Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Bw, Gabriel Migire kwa watumishi kushiriki kwenye michezo, ili waendelea kuleta vikombe zaidi na kuheshimisha Wizara na hata kuongeza ufanisi na tija makazini.
 
Hatahivyo, ameahidi kuongeza bajeti ya michezo na kununua vifaa stahiki, ambavyo TAA watapangiwa na Wizara kununua kwa ajili ya michezo mbalimbali, ikiwemo baiskeli zitakazotumika kwenye mashindano.
Halikadhalika, ameahidi kutembelea kambi ya Klabu ya Sekta ya Uchukuzi, itakayoshiriki kwenye michezo ya Mei Mosi itakayoanza tarehe 14 hadi 29 April, 2023 mkoani Morogoro.
 
Awali Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Bw. Mbura Tenga ameishukuru TAA kwa ushirikiano wao mkubwa wa kutoa wachezaji wengi wanaoshiriki kwenye michezo mbalimbali.
 
“TAA mmekuwa mfano wa kuigwa kwa kutoa wachezaji wengi wenye vipaji ambao wamekuwa chachu ya kuleta ushindi kwenye klabu yetu ikiwa ni moja ya taasisi kubwa tano kati ya 14 zinazounda Sekta ya Uchukuzi, ambapo wapo wachezaji wanaocheza mchezo ya mtu mmoja mmoja na pia kama timu ambayo inatuletea makombe mengi, pamoja na kombe na ushindi wa jumla, hivyo tunawapongeza sana” amesema Bw. Tenga.
 
Bw. Tenga amesema Uchukuzi inatarajia kushiriki kwenye michezo ya soka, netiboli, kamba, riadha, kuendesha baiskeli, karata, bao, draft na mpira wa wavu.

About the author

mzalendoeditor