Featured Kitaifa

ZAIDI YA SH.BILIONI 22 KUJENGA MTANDAO WA BARABARA ZA SEGEREA

Written by mzalendoeditor

Na Angella Msimbira DAR ES SALAAM

ZAIDI ya Sh bilioni 22 zinatarajia kutumika kujenga mtandao wa barabara za Segerea kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 11.55 kupitia Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam(DMDP) awamu ya pili.

Hayo yamebainishwa Machi Mosi, 2023 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Angellah Kairuki alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Majengo, kata ya Vingunguti wakati wa ziara ya kukagua miradi inayotekelezwa katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Amesema barabara zilizotengewa kiasi hicho cha fedha ni barabara ya Barakuda –Chang’ombe – Majichumvi yenye urefu wa kilometa 3.5 itakayojengwa kwa kiwango cha lami, Barabara ya Majumbasita –Segerea pamoja na ujenzi wa Daraja la Pela Pela kwa upande wa Kata ya Vingunguti.

Pia ujenzi wa barabara ya lami ya Depo- Miembeni-Pande-Chambu-Zahanati Vingunguti yenye urefu wa kilometa 2.55 na itagharimu Sh bilioni 5.02.

Amesema barabara nyingine ni Mawenzi- Kisiwani yenye urefu wa kilometa 2.5 itakayojengwa kwa gharama ya Sh bilioni 4.923 kwenye kata ya Tabata ambayo nayo itajengwa kwa kiwango cha lami.

Aidha, Waziri Kairuki amewataka viongozi wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa inazingatia thamani ya fedha na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.

Pia amewataka wahakikishe wanatekeleza kwa uwazi na kuweopo ushirikishwaji na kutoka taarifa kwa wananchi ili waweze kujua miradi inayoendelea katika maeneo yao.

Kairuki pia amewataka kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao na kuendelea kuifuatilia kwa karibu ili ikamilike kwa wakati

About the author

mzalendoeditor