Featured Kitaifa

WANAHABARI GEITA WAMPONGEZA RC SENYAMULE

Written by mzalendoeditor

 

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akipokea hati ya pongezi kutoka kwa  Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari wa  Mkoa wa Geita Bw. Renatus Masuguliko kwa kutambua mchango wake na kuleta mageuzi kwa kipindi ambacho alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita. Hati hiyo ya pongezi amekabidhiwa leo tarehe 19/12/2022 Ofisini kwake Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari wa  Mkoa wa Geita na Chama cha Waandishi wa Habari wa  Mkoa wa Dodoma mara baada ya kupokea hati ya pongezi ya kutambua mchango wake na kuleta mageuzi kwa kipindi ambacho alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita. Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari wa  Mkoa wa Geita Bw. Renatus Masuguliko, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari wa  Mkoa wa Dodoma Bw. Mussa Yusuph, Bw. Novatus Lyaruu Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari wa  Mkoa wa Geita na Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari wa  Mkoa wa Dodoma Ben Bago.

………………………….

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amepokea hati ya pongezi kutoka kwa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Geita kwa kutambua mchango wake na kuleta mageuzi katika kipindi ambacho amekua Mkuu wa Mkoa huo.

Hati hiyo imewasilishwa leo tarehe 19/12/2022 na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Geita Bw. Renatus Masuguliko akiambatana na Katibu wake Bw. Novatus Lyaruu.

Bw. Masuguliko amesema kwa takribani mwaka mmoja ambao Mhe. Mkuu wa Mkoa Bi. Senyamule amekuwa mkoani Geita, amefanikiwa kuleta mabadiliko chanya katika sekta zote na kumpongeza kwa kusimamia kwa vitendo kaulimbiu aliyoianzisha ya “Geita ya dhahabu, Utajiri wa heshima”

“Mkuu wetu wa Mkoa Mhe. Senyamule alivyokuja na hii kaulimbiu mwanzoni hatukumuelewa, lakini kwa kipindi kifupi amefanya mengi katika sekta ya elimu, afya, miundombinu, maji, uchumi na uzalishaji, hivyo watu wa Dodoma mna bahati ya kupata kiongozi mahiri” Amesisitiza Bw. Masuguliko.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule amekishukuru Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Geita kwa kumpa tuzo ya heshima kwa kutambua mchango alioutoa akiwa Geita. 

Amepongeza uongozi wa Chama hicho kwa kuwa mstari wa mbele katika kufanya kazi kwa weledi na maarifa na kusisitiza kuwa kazi hiyo iwe endelevu ili jamii iweze kunufaika na kufahamu mambo ambayo Serikali imekuwa ikitekeleza katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dodoma Bw. Mussa Yusuph na Katibu wake Bw. Ben Bago ambao pia waliambatana na ugeni huo kutoka Geita, wamesema jitahada zinaendelea ili Makao Makuu ya Muungano wa Vyama vya Waandishi wa Habari Tanzania yahamie katika Mkoa wa Dodoma.

About the author

mzalendoeditor