Featured Kitaifa

MVIWA ARUSHA WATAKIWA KUONGEZA UZALISHAJI MZAO YA KILIMO NA MIFUGO.

Written by mzalendoeditor
MRATIBU  wa MVIWAARUSHA Richard Masandika akiongea na waandishi wa habari.
KATIBU Tawala Msaidizi anayeshughulikia viwanda, biashara na uwekezaji mkoa wa Arusha CPA Robert Misungwi akifungua mkutano wa kumi wa mtandao wa vikundi vya wakulima na wafugaji Arusha.
Mwenyekiti wa MVIWAARUSHA Mchungaji mstaafu John Mayo alitoa taarifa ya mtandao huo.
BAADHI ya wakulima na wafugaji wa MVIWAARUSHA wakiwa katika mkutano wao wa kumi.
PICHA ya pamoja ya baadhi ya wakulima na wafugaji kutoka halmashauri sita za mkoa wa Arusha.
…………………………
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
Mtandao wa vikundi vya wakulima mkoa wa Arusha(MVIWAARUSHA) wametakiwa kuendeleza jukumu lao la kuwa walinzi wa uhuru, amani na utulivu wa nchi kwa kuongeza juhudi katika uzalishaji wenye tija wa mazao ya kilimo na mifugo.
Rai hiyo imetolewa na katibu tawala msaidizi anayeshughulikia viwanda, biashara na uwekezaji mkoa wa Arusha CPA Robert Misungwi wakati akifungua Mkutano mkuu wa kumi wa mtandao wa vikundi vya wakulima na wafugaji mkoa wa Arusha(MVIWAARUSHA) ambapo alisema kuwa kwa kuzingatia ukweli palipo na shibe ndipo amani na utulivu vinapata nafasi.
Alisema kuwa kama taifa katika kuendelea kusherehekea miaka 61 ya uhuru hawawezi kutenganisha mafanikio waliyonayo na wakulima pamoja na wafugaji kwani wana mchango mkubwa katika kuleta mafanikio hayo hivyo lazima wathaminiwe na kupewa kipaumbele zaidi.
 “Utulivu na uimara wa kisiasa nchini una uhusiano mkubwa na uhakika wa usalama wa chakula kwani tumbo lenye njaa halijui thamani ya amani na utulivu hivyo endeleeni kuiunga mkono serikali kwa kufanya kazi kwa bidii,”Alisema CPA Misungwi.
Aidha alipongeza MVIWAARUSHA kwa dhamira yao ya kuwaunganisha wakulima na wafugaji katika vikundi na mitandao yao ili kuwawezesha kuzalisha kwa tija na kiuendelevu kwaajili ya kuboresha maisha yao kiuchumi na kijamii ambapo kwa kufanya hivyo wanaunga mkono juhudi za serikali ambayo moja ya majukumu yake ni kuwaleta wananchi maendeleo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa MVIWAARUSHA Mchungaji mstaafu John Mayo alisema kuwa walianzisha mtandao huo mwaka 2001wakiwa na wanachama 200 ambapo mpaka kufikia mwaka huu wa 2022 wapo wanachama 1289 katika vikundi 456 ambapo pia wana mitandao ya msingi 44 na mitandao 6 ya wilaya kutoka Longido, Monduli,Karatu, Arusha DC, Meru na Ngorongoro.
Alisema kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yamekuwa yakiwatatiza kwa kiasi kikubwa katika shughuli za kilimo na ufugaji, imepelekea kutumia njia jumuishi za uzalishaji mali inayojulikana kama kilimo ikolojia ili kuweza kupunguza athari za mabadiliko hayo na kuendeleza utumiaji wa bainowai.
“Dhana hii ya kilimo ikolojia ni muhimu kwani ni rafiki kwa ustawi na uendelevu wa kijamii kiuchumi na kimazingira na MVIWAARUSHA imejidhirisha na kuona kuwa kilimo hichi ni fursa adimu inayopaswa kupewa hadhi stahiki kwa usalama wa mazingira na usalama wa chakula,” Alieleza Mchungaji Mayo.
Alieleza kuwa katika kuendelea kusherehekea miaka 61 ya uhuru na miaka 21 tangu kuadhishwa kwa mtandao huo wanaomba wakulima wathaminiwe zaidi na kutambuliwa rasmi katika mifumo mbalimbali ya uzalishaji pamoja na kuondolewa kwa vikwazo vya kiutawala na kisheria vinavyokwamisha ustawi na maendeleo ya wakulima na wafugaji.
Naye mratibu wa MVIWAARUSHA Richard Masandika alisema kuwa lengo la mkutano huo ni kupata taarifa mbalimbali za maendeleo ya mtanadao huo pamoja na kupeleka taarifa kwa wakulima na wafugaji ili kuweza kuleta uendelevu wa shughuli zao ambapo kwa mwaka huu wa 2022 wana mradi wa Alizeti ambao wakulima wenyewe wanaufanyia utafiti ili kuweza kuainisha mazuri na mabaya katika kazi wanazozifanya.
Alifafanua kuwa pia wana mradi wa uhuwishaji wa ardhi iliyoharibika vibaya kutoka na Arusha kuwa ni eneo la mvua nyingi lakini ardhi yake imechagawanyika kichanga na maeneo ya mwinuko ambayo matokeo yake inapata makorongo na ukame inayoathiri uotaji wa asili wa nyasi na mimea mbalimbali.
“Tuna mradi ambao utafanya kazi ya kuhuisha hali hiyo na kuboresha udongo ili ardhi ipatikane ya kutosha kwaajili ya kilimo na ufugaji kwani azma ya mtandao huo ni kuhakikisha uzalishaji unaenda na utaalamu kwa kuunganisha utaalamu asilia na kufanya kilimo na ufugaji ifuate dhana ya kilimo ikolojia,”Alieleza.

About the author

mzalendoeditor