Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia Viongozi mbalimbali pamoja na Wananchi wa Mkoa wa Lindi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika katika uwanja wa Ilulu Mkoani humo tarehe 01 Desemba, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo Maalum kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainabu Telack kwenye Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika kwenye uwanja wa Ilulu Mkoani Lindi tarehe 01 Desemba, 2022.
……………………..
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan, amewaelekeza wadau wote wa mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na UKIMWI kuweka jitihada na mikakati madhubuti katika kuzuia maambukizi mapya.
Rais Samia ametoa maelekezo hayo leo kwenye maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika katika uwanja wa Ilulu akieleza lengo la mikakati hiyo ni kutokomeza kabisa maambukizi.
Aidha, Rais Samia ameagiza zifanyike jitihada za kuzuia maambukizi mapya kwa makundi maalumu kwenye jamii kwa kuweka mikakati ya kupata fedha za kutosha katika mapambano dhidi ya janga la UKIMWI.
Rais Samia pia amesema kundi la vijana liangaliwe kwa upekee kwa kuwa maambukizi mapya hutokea kwa wenye umri wa miaka 15 – 24, hususan wasichana.
Vile vile, Rais Samia ameitaka Wizara ya Afya kuweka mikakati ya kutokomeza ubaguzi na unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU kwa kutoa elimu ya kutosha kwa watoa huduma za afya, maofisini na katika jamii.
Rais Samia amewataka Viongozi na wananchi kutumia maadhimisho hayo kutafakari kwa kina na kuhakikisha kunawekwa mikakati itakayoimarisha usawa ili kutokomeza maambukizi.