Featured Kitaifa

SERIKALI, WADAU KUSHIRIKIANA USIMAMIZI WA MALEZI YA MTOTO

Written by mzalendoeditor

Asila Twaha, TAMISEMI

Serikali imesema itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kusimamia suala la usimamizi wa malezi ya mtoto kwa kuhakikisha watoto wanafikia hatua ya ukuaji timilifu.

Akimuakilisha Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya Bi. Marim Nkumbwa katika uzinduzi wa Mradi Malezi awamu ya tatu kupitia Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi na Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto uliofanyika leo Jijini Dodoma.

Bi. Mariam amesema lengo la mradi wa malezi awamu ya tatu ni kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto kupitia vituo vya kutolea huduma za afya amesema kuwa, Ofisi ya Rais –TAMISEMI itaendelea kusimamia suala la usimamizi wa malezi ya mtoto kwa kuhakikisha wanaimarisha utoaji wa huduma za elimu na Afya msingi kwa kuweka miundombinu rafiki na inayotosheleza kwa wananchi ikiwemo malezi, makuzi na maedeleo ya awali ya watoto wadogo katika vituo vya kutolea huduma za afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Akifafanua suala la upatikanaji wa takwimu sahihi katika usimamizi wa watoto amesema Ofisi ya Rais -TAMISEMI itaendelea kuweka takwimu na taarifa sahihi za utekelezaji wa mradi kufikia lengo na kuwajengea uwezo watumishi kwenye fani za Afya, Ustawi wa Jamii pamoja na kutoa mafunzo kwa kamati zinazoshughulika na huduma za malezi.

“Mradi huu umeshatekelezwa awamu ya kwanza na pili na kwa kuona maendeleo yake wadau wameendelea kushirikiana na Serikali kuendelea awamu hii ya tatu”

Nitoe rai kwa Mikoa inayoenda kutekeleza mradi ambao ni Mkoa wa Arusha na Tabora ambapo vituo 336 vinaenda kufikiwa katika mradi huu wasimamizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa toeni ushirikiano kwa kufanya vizuri katika utekelezaji muwe mfano mzuri ili mradi huu uweze kutekelezwa na Mikoa mingine.

Awali akimuakilisha Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Nandera Mhando amesema uwepo na uhusiano mzuri kati ya Serikali na wadau kutawezesha kuchangia kwenye jitihada za Serikali katika kutoa huduma za malezi, makuzi na maendeleo ya awali kwa watoto na kuhakikisha watoto wote nchini wanakuwa kwenye mwelekeo sahihi wa kufikia ukuaji timilifu.

Naye Mkurungenzi wa TACDEN Mwajuma Rwebangira ameishukuru Serikali kuendelea kushirikiana na wadau na kuiomba kuendelea kuwasimamia wasimamizi wa mradi kuutekeleza kwa maelengo yaliyokusudiwa ili kuwe na matokeo chanya kwa jamii.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkaazi wa EGPAF Charles Mafoko ameishukuru Serikali kwa ushirikiano wake kutoka kwenye malezi awamu ya kwanza na ya pili. Pia ameeleza kuwa mradi huu utandelea kuchangia jitihada za Malezi awamu ya kwanza na ya pili.

Aidha, mradi wa malezi awamu ya tatu ni ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Wadau wa huduma za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (All ECD Stakeholders)

About the author

mzalendoeditor