Featured Kitaifa

WAZIRI MKUU KUONGOZA HARAMBEE UJENZI WA BASILIKA DODOMA

Written by mzalendoeditor

Kanisa la Kibasilika la Parokia ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo-Kizota Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma ujenzi ukiwa unaendelea ambapo hadi sasa umefikia 24%.

………………………….

Na Ndahani Lugunya,Dodoma.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa Dominika ya tarehe 20 mwezi huu Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme,anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika harambee ya ujenzi wa Kanisa la Kibasilika unaoendelea katika Parokia ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo-Kizota Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Harambee hiyo  Mhe.Mizengo Kayanza Peter Pinda-Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  imeeleza kuwa,Harambee hiyo itafanyika katika Ukumbi wa Land Mark-Kilimani Jimboni Dodoma kuanzia majira ya saa 4:00 kamili asubuhi.

Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa pamoja na mgeni rasmi katika Harambee hiyo  Mhe.Waziri Mkuu Majaliwa,wadau na wageni mbalimbali  pia watashiriki harambee hiyo yenye lengo la kukusanya zaidi ya Tsh Bilioni 1, ili kuendeleza ujenzi wa Kanisa hilo lenye hadhi ya kibasilika ambapo ujenzi wake umefikia hatua ya unyanyuaji wa nguzo.

Akielezea gharama za mradi wa ujenzi wa Kanisa hilo Paroko wa Parokia hiyo Padri Joby Tharayil MCBS amesema kuwa,hadi kukamilika kwake Kanisa hilo linatarajiwa kugharimu takribani Shilingi Bilioni tano,ambapo kiasi cha Shilingi Bilioni moja na Milioni mia mbili zimekwishatumika hadi sasa.

Padri Joby amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutoka ndani na nje ya Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma,kuungana kwa pamoja kushiriki harambee hiyo ili waweze kujichotea Baraka za Mungu kwa kushiriki kumjengea Hekalu.

“Ndugu zangu kama Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa ameamua kuungana na sisi kutushika mkono na kutoongoza kuchangisha fedha kwa ajili ya Kanisa letu kwanini  sasa na sisi tusiungane nae kumpa joto katika zoezi hilo kubwa na la Kimungu atakalolifanya?” amehoji Padri Joby.

Hata hivyo amesema Dodoma ni sehemu ambayo inaweza kuwakusanya watu kutoka Tanzania nzima kwa mwendo  wa usafiri wa siku moja,hivyo uwepo wa Kanisa hilo kubwa utasaidia kuweza kuwakusanya watu  wengi kutoka nchi nzima.

“Ndoto yetu wana Kizota ya kujenga Basilika ni kuwezesha waamini na watu wote kutoka Tanzania  na kwingineko kuchota Baraka sawa kabisa  na zile ambazo wangeweza kuchota kutoka Roma au kwingineko,” Amesema Padri Joby.

Ameongeza kuwa Kanisa hilo linalojengwa lina uwezo wa kuchukua watu 2000 walioketi,ambapo eneo la chini litaweza kuchukua watu 1200 na eneo la juu watu 800,pia litakuwa na altare 15 ndani yake,minara 7  yenye urefu unaokadiriwa kuwa ghorofa tisa.

Aidha Kanisa hilo pia litakapokamilika litakuwa na eneo la chini (Underground) kama Kanisa dogo la kuabudia Sakramenti takatifu saa 24,ambapo kutakuwa na masalia ya Watakatifu 30,huku masalia ya Watakatifu 15 yamewasili hadi sasa Parokiani hapo.

Padri Joby amewataja Watakatifu hao 15 ambao mpaka sasa masalia yao yamekwishawasili Parokiani hapo kuwa ni  masalia ya Mt.Mama Theresa wa Calcutta,Mt.Rita wa Kashia,Mt.Vicent,Mt Lusia,Mt.Anthony,Mt.Bernadetta,Mt.Fransisco wa Sale na Mt.Sesilia.

Masalia mengine ni ya Mt.Luigi Gonzaga, Mt.Theresia wa Mtoto Yesu,Mt.Augustino,Mt.Katarina wa Siena,Mt.Martine,Mt.Fransisco wa Asizi na Mt.Yohane Maria Vianey.

Ikumbukwe kwamba Basilika ni Kanisa lenye hadhi ya juu kabisa ya Makanisa kwa mujibu wa kanuni na taratibu za Kanisa Katoliki,ambapo mfano wa Basilika ni lile la Mt.Petro kule Roma ambako watu wamekuwa wakienda kusali,kuhiji na kupata Baraka maalum.

About the author

mzalendoeditor