Featured Kitaifa

ASKOFU KINYAIYA AONYA WANAUME WANAOPENDA KULELEWA NA WAKE ZAO

Written by mzalendoeditor

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Mhashamu Beatus Michael Kinyaiya OFM Cap,akiwawekea Stola Wanandoa Bwana Amosi na Bibi Devotha katika madhehebu ya utolewaji wa sakramenti hiyo takatifu ya Ndoa.

……………………………….

Na Ndahani Lugunya,Dodoma.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Mhashamu Beatus Michael Kinyaiya amesema kuwa,wajibu mkubwa wa mwanaume alionao katika familia ni kuhakikisha kwamba anamtumza mkewe na familia yake.

Askofu Mkuu Kinyaiya amesema hayo hivi karibuni wakati akitoa homilia yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu ya utoaji wa sakramenti ya Kipaimara kwa waimarishwa 220 sanjari na kubariki ndoa jozi 28 katika Parokia ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili-Bihawana.

Amesema siku hizi kumeibuka tabia ya baadhi ya wanaume wakiwemo vijana ambao wanataka walelewe na wake zao,kwa kukaa kizembe  pasipo kujishughulisha kwa shughuli yoyote ile ya kiuchumi wakisubiri wake zao wakatafute walete, na pindi wanapokuwa wamejipatia fedha huomba fedha hizo kwenda kunywea pombe.

“Ni wajibu wako kujua kwamba mke wako atakula nini watoto watakula nini watavaa nini watalala wapi ni wajibu wako huo.wewe Baba unatakiwa umsaidie mke wako ukatafute ulete na sio kunyoosha mkono kwa mke wako kuomba kile alichokitafuta si sawa hiyo hata kidogo.

Wewe Baba unatakiwa ufikirie hivi likitokea la kutokea kesho mke wangu anaugua,mimi au watoto tutafanyaje.Mtoto anahitaji kwenda Shule anahitaji sare ya Shule na mahitaji mengine mengi ninafanya nini.

Lazima uweke akiba sio unapata kidogo unakula vyote siku hiyo hiyo au unaweka tumboni kwako tu kwa kula nyama choma unarudi nyumbani umelewa unaanza kupiga kelele tu hujaleta chochote hujaweka akiba kwa kesho.na ndiyo maana wengi tunahaingaika kweli ikitokea ugonjwa au mtoto akichaguliwa kwenda Sekondari inakuwa tabu,” amesema Askofu Kinyaiya.

Kutokana na hilo Askofu Mkuu Kinyaiya amewataka wanaume wote kujiwekea utaratibu wa kuweka akiba,ili inapotokea hitaji la haraka na lazima wawe na akiba itakayowasaidia.

“Wewe Baba una wajibu wa kumtunza  Mke wako katika masuala mengine vilevile.huyo mke ni wako sio wa familia yenu wewe mwanaume.huyo mke wako sio wa familia yenu hakuolewa na kila mtu katika familia sio kila mtu anakuja anamfokea mke wako nawewe umekaa kimya kama gogo.

Au wanamnyanyasa unakaa kimya tu Mamaako anamfokea wewe unapita kama husikii Dada zako wanamwambia mke wako ondoka hapa na maneno mengine ya kumbugudhi wewe husikii unajifanya gogo hapana,mtetee mke wako ni wakwako huyo hakuolewa na familia lazima umtetee simama umkingie kifua mke wako.

Tafaadhali naomba wanaume tutimize wajibu wetu na zaidi sana kulinda sifa ya mke wako sio unatoka nje kwa wenzako unaanza kusema siri ya mke wako matokeo yake watu wanakuona wewe ndio hufai,” amesema Askofu Kinyaiya.

Aidha amesema kwamba Mwenyezi alipomuumba Eva kutoka katika ubavu wa Adamu kusudi lilikuwa ni kumfanya kuwa msaidizi na  si vinginevyo, hivyo wajibu wa kwanza wa Mwanaume ni kumpokea mwanamke  kama msaidizi wake na kumsaidia pia.

“Sasa la kwanza la kumsaidia huyu mwanamke ni kiroho ni wajibu wako wewe Baba kuhakikisha mke wako unamsaidia akue kiroho.haiwezekani unaondoka nyumbani kuja Kanisani mke wako amelala tu. unamuuliza Mama unaenda misa ya ngapi anakwambia sina mpango wa kwenda Kanisani nawewe unaamua kuondoka na kumwacha amelala hapo hujatimiza wajibu wako.

Umsaidie mke wako kiroho lakini ili uweze kumsaidia mke wako kiroho lazima nawewe ujue una Kiongozi wako ambaye ni lazima umsikilize maongozi yake ambaye ni Mwenyezi Mungu.lazima uchote busara na nguvu kwake ili uweze kuongoza mke wako na nyumba yako muhimu sana hilo,” Amesema.

Sanjari na wanaume,amewataka wanawake kutambua kwamba pamoja na wao kuitwa kuwa wasaidizi wa waume zao,lakini haina maana kuwa wakae na kubweteka nyumbani pasi na kujishughulisha kwa chochote.

Pamoja na wajibu huo Askofu Mkuu Kinyaiya amesema wajibu mwingine msingi wa mwanamke ni kuheshimu ndugu wa mume wake.

“Na wale Ndugu wa mume wako waheshimu hawakukuoa wewe lakini waheshimu.na ukiona kitu hakiendi mwambie mumeo taratibu kwamba naona hapa baadhi ya mambo  hayaendi sawa. dada zako wamekuwa waongeaji sana kwa hiyo waambie wapunguze.

Mwambie ukweli sio unagombezwa na wengine unakuja kumnunia mumeo wapi na wapi.kwamba huyo mama yako kazidi hapana mwambie taratibu mtafute namna ya kutatua matatizo yaishe,”amesema Askofu Kinyaiya.

Aidha Askofu Mkuu Kinyaiya amesisitiza zaidi suala la wanandoa kutenga muda wa kukaa pamoja kwa ajili ya mazungumzo,ili kuweka sawa mambo yao kama wanandoa.

“Unajua mume wako anapokuoa kuna vitu ameona ndani yako sasa hakikisha unaendelea navyo.kama alikuona ni msafi unaongea vizuri una heshima endelea navyo. utakapogeuka uanze kuwa mchafumchafu huna heshima lazima mumeo atajiuliza tu kwamba mwanamke niliyemuoa ndo huyu kweli.kwa hiyo akina Mama mkae vizuri wanaume wenu waendelee kuwapenda,” amesema.

Waimarishwa hao 220 wa Mapaji Saba ya Roho Mtakatifu, ni kutoka katika Vigango jirani na Parokia hiyo, ikiwemo Kigango cha Mt.Anthony wa Padua- Mbabala, Mpalanga, Nkhome, Chididimo, Chizomoche na Kigango Mama cha Bihawana.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Mhashamu Beatus Michael Kinyaiya OFM Cap,akiwawekea Stola Wanandoa Bwana Amosi na Bibi Devotha katika madhehebu ya utolewaji wa sakramenti hiyo takatifu ya Ndoa.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Mhashamu Beatus Michael Kinyaiya OFM Cap,akitoa sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa mmoja kati ya waimarishwa 200 waliopata sakramenti hiyo,katika Parokia ya ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili-Bihawana.(Picha zote na Ndahani Lugunya)

About the author

mzalendoeditor