WAZIRI wa Maliasili na utalii Balozi Dkt Pindi Chana akiongea na waandishi wa habari jijini Arusha juu ya mkutano wa UNWTO unatarajiwa kuanza kesho.
………………………………
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan anatarajia kufungua mkutano wa kimataifa wa 65 wa shirika la utalii duniani(UNWTO) unatarajiwa kufanyika kesho Oktoba 5,2022 jijini Arusha
Akiongea na waandishi wa habari Waziri wa maliasili na utalii,Balozi Dkt.Pindi Chana alisema kuwa mkutano huo utakuwa chachu ya kukutana na wadau mbalimbali wakiwemo wataalam wa utalii na ukarimu katika ngazi ya kimataifa na kikanda,watoa huduma kwenye mnyororo wa utalii,wawekezaji pamoja na watu mashuhuri zaidi ya 150.
Alisema pia utawezesha kujengea uwezo wataalam wao na wadau wa utalii katika kutangaza utalii,kuendeleza na kufungamanisha mazao ya utalii katika kanda mbalimbali za utalii nchini kulingana na shabaha yao ya kuongeza idadi ya watalii milioni tano na mapato ya dola za marekani bilioni sita ifikapo mwaka 2025.
“Mkutano huu ni fursa adhimu ya kukuza uchumi wa jiji la Arusha ,mikoa ya jirani na Tanzania kwa ujumla hivyo anatoa rai kwa wananchi katika kuchangamkia fursa zitakazotokana na mkutano huu,”alisema
Sambamba na hayo alisema kuwa mkutano huo utahudhuriwa na Katibu mkuu wa shirika la UNWTO Zurab Pololikashvili pamoja na kukutanisha mawaziri wenye dhamana ya masuala ya utalii na maliasili kutoka nchi wananchama wa UNWTO wa kanda zaidi ya 50 kujadili kuhusu mustakabali wa ustawi wa maendeleo ya sekta ya utalii barani Afrika hasa baada ya athari za mlipuko wa janga la Uviko 19.
Alisema kuwa pia kutafanyika matukio mbalimbali ambayo ni pamoja na jukwaa la uwekezaji kwa ajili ya kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini ambapo pia itazinduliwa Investment Guideline(Tourism Doing Business) sambamba na Marketing Symposium kwa ajili ya kuwajengea uwezo wadau wa utalii kuhusu masuala ya masoko.
” Pia kutafanyika uzinduzi wa A tour of African Gastronomy pamoja na ziara za mafunzo(FAM Trips) ambapo watapata nafasi ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania ikiwemo Hifadhi ya Ngorongoro,Jumuiya ya wanyama pori ya Buruge na city Tour ya vivutio mbalimbali katika jiji la kitalii la Arusha,”alisema.
Waziri Chana alisema kulingana na sera ya Taifa ya utalii ya mwaka 1999 mkutano huo ni muhimu kwa kuwa ni mojawapo ya jitihada za serikali katika kuongeza idadi ya watalii nchini pamoja na kutanua wigo wa mazao ya utalii nchini kupitia uendelezaji wa mazao ya utalii kimkakati hususani utalii wa mikutano.
Mkutano huo unaenda sambamba na kauli mbiu ya Rebuilding Africa’s Tourism Resilience for inclusive socio Economic Development.