Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) inashirkiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) katika kutekeleza program na miradi mbalimbali ya hifadhi na usimamizi wa mazingira inayotekelezwa chini ya mikataba ya kimataifa.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati akijibu maswali bungeni jijini Dodoma leo Septemba 13, 2022.
Katika swali la msingi Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Maryam Azan Mwinyi alitaka kufahamu Serikali ina mkakati gani wa kuunda kikosi kazi kuratibu Mikataba ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Mhe. Khamis alisema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi mwanachama wa Mikataba mbalimbali ya kimataifa ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ambayo inaratibiwa chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais.
Aliongeza kuwa utaratibu unaotumika katika kuratibu masuala ya mikataba ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivyo naibu waziri huyo alifafanua kuwa utaratibu huo ni wa kushirikiana katika majadiliano, pamoja na kushiriki katika mikutano ya kimataifa na utekelezaji wa mikataba hiyo.
Aidha, alisema kuwa majadiliano yanayoshrikisha pande mbili za Muungano katika masuala ya mazingira na mikataba yua kimataifa yapo kwa mujibu wa sheria na kuwa mawaziri wa pande hizo mbili wanakutana na kujadiliana.
Kwa upande mwingine alitaja miradi ya kimazingira inayotekelezwa kwa upande wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kuwa ni Mradi wa ujenzi wa kuta za kupunguza kasi ya maji ya bahari Mtwara Mikindani na Wilaya ya Kaskazini A, Zanzibar.
Pia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) unaotekelezwa Wilaya ya Mvomero (Morogoro), Simanjiro (Manyara), Kaskazini A (Unguja). Kishapu (Shinyanga) na Mpwapwa (Dodoma).
Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na kuongeza Usalama wa Chakula katika maeneo kame Tanzania (LDFS) unatekelezwa katika Wilaya ya Nzega (Tabora), Kondoa (Dodoma), Mkalama (Singida), Magu (Mwanza) na Micheweni (Pemba).