Featured Kitaifa

SERIKALI KUANZA UJENZI WA VYUO VYA VETA KATIKA WILAYA 62

Written by mzalendoeditor

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatarajia kuanza ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya 62 ambazo hazina vyuo hivyo.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga (Mb) katika kikao na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii cha uwasilishaji wa utekelezaji wa mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko 19 kilichofanyika Septemba 6, 2022 Jijini Dodoma

Mhe. Kipanga ameieleza Kamati hiyo kuwa katika Mwaka wa Fedha 2022/23 Wizara imetenga jumla ya Shilingi bilioni 100 ambazo zitawezesha kujenga majengo muhimu katika vyuo hivyo ili kuviwezesha kuanza kutoa mafunzo katika maeneo hayo.

“Kwenye bajeti ya Wizara ya mwaka huu wa fedha tumetenga Shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa majengo muhimu katika Wilaya zote ambazo bado hazina vyuo vya VETA ili vianze kutoa mafunzo,” amefafanua Mhe. Kipanga

Ameongeza kuwa vyuo hivyo vikikamilika vitawezesha Wilaya zote nchini kuwa na vyuo vinavyotoa mafunzo ya ufundi na ufundi stadi ambapo mpaka sasa tayari kuna vyuo 73 vikiwemo vya Wilaya na mikoa.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Stanslaus Nyongo (Mb) amesema Kamati imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo na kuipongeza Wizara.

Amesema katika taarifa iliyotolewa kwa Kamati inaonyesha miradi yote iliyokuwa katika Mradi wa UVIKO 19 imekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 jambo ambalo linaonyesha kuwa imekamilika kwa kiwango kikubwa.

About the author

mzalendoeditor