Featured Kitaifa

WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI YAANDAA MPANGO WA KUWAWEZESHA VIJANA KUJIAJIRI 

Written by mzalendoeditor

Na Mbaraka Kambona,

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeandaa vituo atamizi vinne kwa ajili ya kuwafundisha vijana unenepeshaji wa mifugo ili waweze kujiajiri na kujiongezea kipato kupitia Sekta ya Mifugo.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki Agosti 24, 2022 wakati akitoa taarifa kwa umma ya kuwataka vijana kujitokeza kuomba nafasi za kujiunga katika Vituo Atamizi vilivyoandaliwa Mkoani Tanga, Mwanza na Kagera.

Alisema Mhe. Rais Samia anataka kuona vijana wanawezeshwa kujiajiri kupitia Sekta ya Mifugo kwani fursa zilizopo katika sekta hiyo ni nyingi ambazo zinaweza kuwasaidia vijana kujiongezea kipato na kukuza uchumi wa taifa.

Aliongeza kwa kusema kuwa wanaanzisha vituo hivyo kuwafunza vijana kufanya ufugaji kwa njia ya vitendo ili waweze kutumia ujuzi huo kujiajiri na kujiongezea kipato.

“Hawa vijana 240 watakaokuwa katika vituo hivyo vilivyoandaliwa wataelimishwa namna ya kufanya ufugaji wa kibiashara ili waweze kusaidia kuwabadilisha wafugaji wengine kufanya ufugaji wa kisasa na wenye tija na kuondokana na ufugaji wa kujikimu”, alisema

Halikadhalika, alisema kuwa ufugaji wa kibiashara watakaofanya vijana hao utasaidia kuongeza uhakika wa kupatikana kwa malighafi katika viwanda lakini pia kuvitumia vituo hivyo kuleta mageuzi katika sekta ya ufugaji.

Aidha, Waziri Ndaki alisema kuwa vijana wataokuwa tayari kujiunga na vituo hivyo nafasi zimeshatangazwa kupitia tovuti ya Wizara na fomu zinapatikana humo, hivyo wafanye hima kwani mwisho wa maombi hayo kupokelewa ni Septemba 7, 2022.

Sifa za muombaji awe raia wa Tanzania, awe ni mhitimu wa mafunzo ya mifugo katika ngazi ya Astashahada, Stashahada au Shahada kutoka vyuo vinavyotambuliwa na serikali na awe na umri kati ya miaka 18-30.

Jitihada hizo za Wizara ni sehemu ya utekelezaji maagizo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa Agosti 8, 2022 ambapo aliielekeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inashirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuwawezesha vijana kujiajiri ili kujiongezea kipato kupitia Sekta ya Mifugo.

About the author

mzalendoeditor