Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari kuhusiana na Mkutano wa Tatu wa Nchi zinazozalisha Madini ya Almasi Afrika (ADPA) uliofanyika katika ukumbi wa AICC uliopo Jijini Arusha
Baadhi ya wataalamu wakiwa kwenye Mkutano wa Tatu wa Nchi zinazozalisha Madini ya Almasi Afrika (ADPA) katika ukumbi wa AICC uliopo Jijini Arusha
…………………………………..
Asteria Muhozya, Tito Mselem na Steven Nyamiti, Arusha
Uenyekiti wa Tanzania kwa Nchi Zinazozalisha Almasi Afrika (African Diamond Producers Association-ADPA) umeonesha kuzaa matunda baada ya kuwezesha kuharakisha kurekebishwa kwa mifumo na nyaraka muhimu za umoja huo.
Nyaraka hizo ni pamoja na Katiba, Kanuni na Miongozo inayosimamia Jumuiya hiyo ambapo mfumo mpya utawezesha kusimamia ipasavyo masuala yanayohusu madini ya almasi na kuleta tija zaidi kwa nchi wanachama.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko Julai 28, 2022, wakati akizungumza na vyombo vya Habari jijini Arusha kuelezea kuhusu uwepo wa mkutano wa Tatu (3) wa Dharula wa nchi zinazozalisha Almasi Afrika, huku Tanzania ikiwa nchi Mwenyeji na Mwenyekiti wa Mkutano huo.
Waziri Biteko ameongeza kuwa, nafasi ya uenyekiti wa Tanzania imewezesha Jumuiya hiyo kupata nafasi ya kualikwa katika Baraza la Umoja wa Mataifa ambapo Tanzania iliiwakilisha Jumuiya hiyo kama Mwenyekiti jambo linalopelekea kuweka msukumo wa masuala yanayohusu wazalishaji wa madini hayo Afrika.
Tanzania ilisaini mkataba wa kujiunga na jumuiya hiyo mwaka 2006 na tangu kipindi hicho imeendelea kuwa mwananchama mzuri ambapo mwaka 2021, ilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la ADPA kwa kipindi cha miaka miwili na inatarajia kukabidhi nafasi hiyo kwa nchi ya Jamhuri ya Zimbambwe mwezi Machi, 2023.
Ameongeza kuwa, madini ya almasi ni miongoni mwa madini yenye urasimu mkubwa wa kibiashara na mnyororo mrefu hivyo, wajibu wa jumuiya hiyo ni kusimamia madini hayo ili kuwezesha kuwepo kwa sauti moja, kuwezesha biashara ya almasi kusonga mbele na pia kuziwezesha nchi wanachama kunufaika na rasilimali hiyo.
Akizungumzia nafasi ya Tanzania katika kusimamia madini hayo, Waziri Biteko amesema kuwa Serikali imefanikiwa kuboresha Mkataba katika Mgodi wa Almasi wa Williamson Diamond uliopo Mwadui, mkoani Shinyanga kwa kuongeza idadi za hisa zinazomilikiwa na Serikali kutoka asilimia 25 hadi kufikia 35.
Kuhusu uzalishaji wa madini hayo amesema kuwa, mgodi huo ulisimamisha uzalishaji kwa muda kutokana na ukarabati hata hivyo uzalishaji wa almasi umerejea tena na kueleza kwamba, uzalishaji wa awali umewezesha kuzalishwa kwa almasi ya pinki yenye uzito wa gramu sita (6) zenye thamani ya Dola za Marekani milioni kumi na mbili.
‘’Tumepata bahati ya kuweka rekodi mwadui na tunatazamia kuzalisha almasi za pinki katika mgodi huo.’’
Akizungumzia historia ya Tanzania katika uzalishaji wa madini ya almasi amesema uzalishaji wa juu wa almasi ulitokea Mwaka wa Fedha 2019/2020 kwa kuzalisha zaidi ya carat 500,000 ambapo imevunja rekodi iliyowekwa mwaka 1977 ya kuzalishwa kwa carat 377,000. Kwa upande wa Soko la Tanzania kwa madini hayo, Waziri Biteko amesema hivi sasa soko la Tanzania kwa madini hayo liko Antwerp nchini Ubelgiji na inaangalia uwezekano wa kuwa na soko lingine Umoja wa Falme za Kiarabu- Dubai ambapo tayari serikali imekwenda kuangalia soko la madini hayo.
“Sasa bei ya almasi imeanza kupanda tena baada ya kushuka kutokana na kuwepo changamoto ya janga la Ugonjwa wa Uviko-19,’’ amesema Waziri Biteko.
Jumuiya ya ADPA inajumuisha nchi kumi na nane (18), ambapo kumi na mbili (12) ni wanachama na sita (6) ni waangalizi. Nchi wanachama ni Angola, Botswana, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ghana, Guinea, Namibia, Sierra Leone, South Africa, Tanzania, Togo na Zimbabwe. Nchi waangalizi ni Algeria, Jamhuri ya Kongo (Brazaville), Gabon, Ivory Coast, Liberia, Mali na Mauritania.
MKutano wa Tatu wa Dharula wa Baraza la Mawaziri umetangauliwa na mkutano wa wataalam kutoka nchi husika chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Adolf Ngunguru. Wataalam hao wanajadili nyaraka mbalimbali zinazohusiana na ADPA kabla ya kuwasilishwa kwenye mkutano wa Baraza la Mawaziri la jumuiya hiyo utakaofanyika Julai 29, 2022.