Featured Kitaifa

BALOZI UMOJA WA NCHI ZA ULAYA AMTEMBELEA JAJI MKUU

Written by mzalendoeditor
Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) Tanzania, Mhe. Manfredo Fanti  (kushoto) akizungumza jambo alipokutana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 28 Julai, 2022 ofisini kwake katika jengo la Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (kushoto) akiwa na Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) Tanzania, Mhe. Manfredo Fanti walipokutana ofisini kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifafanua jambo mbele ya mgeni wake, Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) Tanzania, Mhe. Manfredo Fanti  (hayupo kwenye picha).
Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) Tanzania, Mhe. Manfredo Fanti akimweleza jambo mwenyeji wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo kwenye picha).
Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) Tanzania, Mhe. Manfredo Fanti (katikati) akiwa katika mazungumzo na wenyeji wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (kushoto).
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia), pamoja na Makatibu wa viongozi wakuu wa Mahakama, Katibu wa Jaji Mkuu, Mhe. Venance Mlingi (kushoto) na Katibu wa Jaji Kiongozi, Mhe. Obadia Bwegoge (katikati) wakifuatilia mazungumzo kati ya Mhe. Prof. Juma na Balozi Fanti (hawapo kwenye picha).
Mchumi Mwandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Said Nyenge (kushoto), Msaidizi wa Balozi Fanti, Bi Salome Matuja (katikati) na Msaidizi wa Jaji wa Mahakama, Mhe. Joyce Karata (kulia) wakifuatilia mazungumzo hayo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kushoto) akimwonyesha Balozi  Fanti (kushoto) nakala moja ya Juzuu baada ya mazungumzo yao. Wanaoshuhudia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (wa pili kulia) na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia).
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kushoto) akimwonyesha Balozi  Fanti (kushoto) nakala moja ya jarida la Mahakama la Haki Bulletin, huku Mhe. Siyani (wa pili kulia) na Prof. Ole Gabriel (kulia) wakishuhudia.
Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) Tanzania, Mhe. Manfredo Fanti (kushoto) akimwonyesha mwenyeji wake Jaji Mkuu wa Tanzania (wa pili kushoto) nakala ya chapisho alilokuja nalo kutoka ofisini kwake. Wanaoshuhudia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (wa pili kulia) na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia). 
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kushoto) akibadilishana mawazo na mgeni wake, Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) Tanzania, Mhe. Manfredo Fanti.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na mgeni wake, Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) Tanzania, Mhe. Manfredo Fanti (wa pili kulia) na viongozi wengine waandamizi wa Mahakama, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia). 
(Picha na Faustine Kapama-Mahakama)
………………………………………
 
Na Mary Gwera, Mahakama

Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) Tanzania, Mhe. Manfredo Fanti leo tarehe 28 Julai, 2022 amemtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali ya utoaji haki nchini.

Akizungumza na Jaji Mkuu ofisini kwake katika jengo la Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam, Balozi Fanti amesema kuwa dhumuni mojawapo la kuonana na Mkuu huyo wa Mhimili ni pamoja na kuangalia maeneo mbalimbali ya kushirikiana katika suala zima la kuboresha utoaji haki.

“Moja ya sababu ya kukutana na wewe leo ni pamoja na kufanya mazungumzo ili kufahamu malengo yenu kama Taasisi, changamoto mlizonazo pamoja na kujenga ushirikiano baina yetu,” amesema.

Ameongeza kuwa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) upo tayari kushirikiana na Mahakama ya Tanzania katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuboresha huduma za utoaji haki, hivyo ujio wake umelenga katika kubaini maeneo yenye changamoto yanayowakabili.

Kwa upande wake,  Jaji Mkuu amemueleza Balozi huyo kuwa Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika uboreshaji wa huduma mbalimbali ikiwemo matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), miundombinu ya majengo ya Mahakama na uondoshaji wa mashauri.

“Mahakama ya Tanzania tumekuwa tukitekeleza Mpango Mkakati (2015/2016-2019/2020 na 2020/2021-2024/2025) pamoja na Mradi wa Maboresho wa Huduma za Mahakama unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, yote ikiwa inalenga kuboresha zaidi huduma za Mahakama kwa wananchi,” amesema Mhe. Prof. Juma.

Jaji Mkuu amesema kuwa matumizi ya TEHAMA yamesaidia katika kurahisisha shughuli mbalimbali za Mahakama, huku akitoa mfano kuwa wakati janga la Korona lilipoanza Mahakama haikusimamisha shughuli zake, bali iliendelea kusikiliza mashauri kwa njia ya Mkutano Mtandao ‘Video Conference’.

Aidha, Mhe. Prof. Juma amemweleza Balozi huyo kuwa katika kushughulikia masuala ya familia na hususani haki za wanawake, wameamua kuanzisha Mahakama maalum iliyopo katika Wilaya ya Temeke kwa lengo la kushughulikia kwa karibu masuala hayo.

Ameongeza kuwa miongoni mwa vipaumbele ambavyo Mahakama inasisitiza katika kuangalia njia za haraka zaidi zitakazosaidia kupunguza mlundikano wa mashauri ni pamoja na kutumia Usuluhishi ‘mediation’, uanzishwaji wa Mahakama ndogo zitakazosaidia kusikiliza na kuamua mashauri ya kibiashara.

Hata hivyo, Jaji Mkuu amemueleza Balozi huyo kuwa ingawa Mahakama imepiga hatua katika uboreshaji wa huduma zake, bado kuna changamoto kadhaa ambazo inakabiliana nazo ikiwemo namna ya kufikisha huduma za utoaji haki kwa wananchi ambapo amefafanua kuwa baadhi ya maeneo kukosa majengo ya Mahakama au kuwa mbali na Mahakama.

About the author

mzalendoeditor