Naibu waziri wa kilimo Antony Mavunde akiongea katika maonyesho ya kilimo yaliyofanyika Arusha.
Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt.Geofrey Mkamilo akiongea katika maonyesho ya kilimo yaliyofanyika Arusha.
…………………………..
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
SERIKALI kupitia wizara ya kilimo imekuja na mpango mkakati wa kutengeneza ajira kwa vijana zaidi ya milioni 2.5 ujulikanao kama “Toboa na kilimo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Akizungumza katika maonyesho ya kilimo biashara yalifanyikia katika makao makuu ya kituo cha utafiti wa mbegu kanda ya kaskazini (TARI ) yaliyopo jijini Arusha, Naibu waziri wa kilimo,Antony Mavunde alisema mpango huo ni mwarobaini wa changamoto ya ajira kwa vijana milioni tatu nchini.
Alisema kwa mujibu wa taarifa za nguvu kazi nchi ya Tanzania ina watu wa kufanya kazi milioni 23 ikiwa asilimia zaidi ya 67 ni vijana.
“Na sisi tunaamini tukiwasaidia vijana katika sekta ya kilimo nchi yetu itapiga hatua mara dufu katika kukuza kilimo nchini na kufikia malengo asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 hivyo mpango huo unaanza mwaka huu wa fedha 2021/2022,”alisema.
Mavunde alisema vijana sio kwamba hawapendi kilimo hapo awali kulikuwepo changamoto ya upatikanaji wa ardhi lakini sasa wizara itatafuta maeneo kwa niaba ya vijana sambamba na kuisafisha pamoja na kuweka miumbombinu mbalimbali ya kilimo.
Naibu waziri alisema programu hiyo wanaianza mkoa wa Dodoma wilayani Chamwino na Bahi kwa ajili ya majaribio hivyo wamenza hekari 21000 kwa kuanzia na wizara ya kilimo wataisafisha na kuwapatia vijana kwa ajili ya kuendesha kilimo pamoja na kuwatafutia masoko.
Mavunde alisema serikali inampango mkakati wa kusajili wakulima wote nchi ili kuondokana na changamoto ya wadanganyifu kwani watatoa ruzuku za mbolea kwa kila mkulima aliyesajiliwa ili waweze kunufaika na kilimo wanacholima.
“Kuna baadhi ya wadanganyifu walinufaika kupitia mgongo wa mkulima na hivi sasa tutaangalia takwimu zote zinazomuhusu mkulima husika lakini kwa upande wa huduma za ugani bado kuna changamoto ya uhaba wa maafisa ugani,”alisema Mavunde.
Aliongeza kuwa nchini kunauhitaji wa maafisa ugani 20000 lakini waliopo ni 7000 hivyo wataendelea kuajiri ili kuondokana na changamoto za uhaba wa Maafisa ugani nchini.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TARI,Dkt.Geofrey Mkamilo alisema kupitia wizara na taasisi zake zote wataendelea kuongeza nguvu pamoja na kufanya kazi na maafisa ugani hata katika maeneo ya vijijini.
“Kama mnavyofahamu wizara yetu inamazao mengi ya kimkakati ikiwemo mazao ya mafuta na ili kuweza kufanikisha hilo ni kuhakikisha tunaongeza tija katika uzalishaji ili kuondokana na changamoto ya uagizaji wa mafuta ya kupikia kutoka nje,”alisema Dk.Mkamilo.
Mwakilishi wa katibu tawala mkoa wa Arusha ambaye ni Afisa kilimo mkoani hapa,Daniel Loiruck alisema katika uhitaji wa kilimo ifikapo 2030 kukua kwa asilimia 10 wanahitaji wadau mbalimbali katika mnyororo wa thamani ili kuweza kufikia malengo hayo.
“Kiukweli hii ni indicator muhimu ya public private partnership kwa maana kwamba tunahitaji sekta binafsi katika maeneo yote muhimu ya msingi na ili kuhakikisha haya yote tunayafikia sawasawa ni vyema wizara ya kilimo kwa ikashirikiana wa wadau,”alisema Loiruck.
Mmoja wa wakulima wadogo,Julius Mollel Alieleza kuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya maafisa ugani kutowasaidia wakulima ipasavyo katika masuala ya kilimo pamoja na gharama za ununuzi wa pembejeo za kilimo(mbolea).