Alhamisi, Novemba 26, 2026
HABARI MPYA
Kitaifa

WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA NA MAADILI KATIKA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YAO

 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Mhandisi Benedict Benny Ndomba, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wapya wa e-GA yaliyofanyika  jijini Dodoma,

Na.Mwandishi Wetu.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Mhandisi Benedict Benny Ndomba, amewataka watumishi wapya wa umma kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuongeza ufanisi, uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wapya wa e-GA yanayofanyika jijini Dodoma, Ndomba amesema kuwa watumishi wanapaswa kutumia ujuzi wanaoupata kupitia mafunzo hayo kuboresha utendaji wao wa kazi na kuzingatia misingi ya maadili ya utumishi wa umma ili kuhakikisha huduma za Serikali zinatolewa kwa ufanisi zaidi.

Amesema kuwa e-GA itaendelea kuboresha mifumo ya TEHAMA inayotumika katika shughuli mbalimbali za Serikali ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Aidha, Ndomba amesisitiza umuhimu wa kuzingatia usalama na usiri wa taarifa za ofisi, akieleza kuwa watumishi wanapaswa kulinda taarifa za kikazi na kuepuka kuzitoa nje ya ofisi bila kufuata taratibu zinazotakiwa ili kulinda usalama wa taarifa za taasisi.

Naye, mwezeshaji na mkufunzi wa mafunzo hayo, Bw. Gasper Kisinza, amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea watumishi uelewa kuhusu Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298, pamoja na Kanuni zake za mwaka 2022, kwa kuwafahamisha mambo muhimu ya kisheria na kiutendaji wanayopaswa kuyazingatia katika utumishi wao.

“Watumishi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa, bila upendeleo, ubaguzi wala ubinafsi, ili kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi na taasisi wanazozihudumia,” amesema Kisinza.

Kwa upande wake, Ephraim Sangura, ambaye ni mshiriki wa mafunzo hayo, amesema kuwa mafunzo hayo yataongeza tija katika utendaji wao wa kazi kwa kuwasaidia kufahamu miundo ya Serikali, utunzaji wa nyaraka muhimu za taasisi pamoja na sheria na kanuni zinazohusiana na utumishi wa umma.

Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea watumishi wapya uelewa kuhusu sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma, pamoja na kuwapatia maarifa ya msingi kuhusu e-GA na majukumu yake. Mafunzo hayo ya siku tatu yanatarajiwa kuhitimishwa kesho, Novemba 27, 2026, jijini Dodoma.