NAIBU Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege Qwaray,akizungumza wakati akifungua Kikao Kazi cha Saba cha Kubadilishana Uzoefu baina ya Ofisi ya Rais – Utumishi, Taasisi Simamizi za Maadili ya Utendaji na Mamlaka Simamizi za Maadili ya Kitaaluma, kilichofanyika leo Novemba 26, 2026,Mji wa Kiserikali Mtumba jijini Dodoma.
Na Alex Sonna,MZALENDO BLOG-DODOMA
NAIBU Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege Qwaray, amezitaka taasisi za umma kuimarisha usimamizi wa maadili, uadilifu na uwajibikaji kwa kuweka mifumo madhubuti ya kuzuia na kudhibiti vitendo vya ukiukwaji wa maadili katika utumishi wa umma.
Aidha, ametoa maagizo matano kwa taasisi zinazosimamia maadili ya utendaji na mamlaka za maadili ya kitaaluma, akizitaka kuimarisha ushirikiano, kuwajengea uwezo watumishi, kufanya tathmini za uadilifu na kuongeza matumizi ya mifumo ya Serikali Mtandao ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe.Qwaray ametoa maagizo hayo, wakati akifungua Kikao Kazi cha Saba cha Kubadilishana Uzoefu baina ya Ofisi ya Rais – Utumishi, Taasisi Simamizi za Maadili ya Utendaji na Mamlaka Simamizi za Maadili ya Kitaaluma, kilichofanyika leo Novemba 26, 2026,Mji wa Kiserikali Mtumba jijini Dodoma.

Amesema licha ya juhudi za Serikali kuimarisha mifumo ya kidijitali katika usimamizi, udhibiti na utoaji wa huduma, bado kuna viashiria vya ukiukwaji wa maadili vinavyojitokeza katika taasisi za umma, hali inayohitaji ushirikiano na hatua madhubuti za kukabiliana navyo.
“Baadhi ya vitendo hivyo kuwa ni rushwa, uvujishaji wa siri za Serikali, matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za umma, hujuma dhidi ya miradi ya maendeleo, matumizi ya lugha zisizo na staha, upendeleo na ukosefu wa uzalendo.”amesema Mhe.Qwaray
Mhe.Qwaray amesema watumishi wa umma wanapaswa kutambua kuwa wanatekeleza majukumu yao kwa niaba ya Rais, hivyo mwenendo na maamuzi yao yanaakisi taswira ya Serikali mbele ya wananchi.
“Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji kuwa na rasilimaliwatu yenye uadilifu, weledi, uzalendo na uwajibikaji ili kufanikisha malengo ya Taifa na kuleta ustawi wa wananchi.”amesisitiza

Katika maagizo hayo Mhe.Qwaray amezitaka taasisi husika kuhakikisha maazimio ya vikao vya kubadilishana uzoefu yanatekelezwa, kuendeleza mafunzo ya maadili kwa watumishi, kuhakikisha kila mtumishi anapata na kuelewa Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma pamoja na kuimarisha matumizi ya Hati ya Ahadi ya Uadilifu.
Pia amezitaka taasisi hizo kuhamasisha matumizi ya Serikali Mtandao katika utoaji wa huduma, kuhakikisha kila mtumishi anakuwa na anuani rasmi ya barua pepe ya kikazi na kufanya tathmini pamoja na tafiti za mara kwa mara ili kubaini changamoto za uadilifu na kuchukua hatua stahiki.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuweka mifumo rafiki ya kupokea na kushughulikia mrejesho wa wananchi pamoja na kuhakikisha miongozo na nyaraka za kimaadili zinapatikana kwa urahisi kupitia tovuti rasmi za taasisi husika.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Leila Mavika, amesema taasisi na mamlaka zinazosimamia maadili zinapaswa kuongeza usikivu, uwazi na uwajibikaji ili kujenga utamaduni wa uadilifu na kuimarisha imani ya wananchi kwa serikali.
Mavika amesema kikao hicho cha siku mbili ni jukwaa muhimu la kubadilishana taarifa, uzoefu na maarifa kati ya taasisi zinazohusika na usimamizi wa maadili, pamoja na kujengeana uwezo kuhusu namna bora ya kusimamia maadili ya kisekta na kuboresha huduma zinazowafikia wananchi moja kwa moja.

Amebainisha kuwa taasisi hizo zina wajibu wa kusimamia misingi ya sheria, uwazi, uwajibikaji, haki na usawa, sambamba na kupinga vitendo vya rushwa na ukiukwaji mwingine wa maadili unaoweza kuathiri maslahi ya umma.
Ameongeza kuwa washiriki wa kikao hicho wanapata fursa ya kujifunza kutoka kwa wataalamu wa wizara na taasisi mbalimbali, zikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Afya pamoja na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Kwa mujibu wa Mavika, ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha changamoto za kimaadili zinazojitokeza katika sekta mbalimbali zinapatiwa ufumbuzi na kwamba uwajibikaji unakuwa sehemu ya utamaduni wa kila taasisi ya umma.

Naye Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Patient Ntwina, amesema maelekezo yaliyotolewa na mgeni rasmi yanapaswa kugeuzwa kuwa maazimio na kutekelezwa katika taasisi husika ili kuimarisha maadili katika maeneo ya kazi.

Amesema vikao hivyo vinatoa fursa kwa taasisi kubadilishana uzoefu na kupata nyenzo za kuboresha usimamizi wa maadili, akisisitiza umuhimu wa washiriki kuyafikisha maarifa wanayopata kwa watumishi wengine ili yaonekane kwa vitendo.


