Featured • Kitaifa

VITABU VYA MALEZI NA HUDUMA ZA WATOTO NJITI VYAZINDULIWA

Written by Alex Sonna

 

Serikali kwa kushirikiana na Taasisi ya Doris Mollel Foundation (DMF) imezindua vitabu vitatu vinavyolenga kuimarisha malezi na huduma kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (watoto njiti), kwa kuwajengea uwezo wazazi, wahudumu wa afya na wadau wanaohusika na huduma za watoto wachanga.

Uzinduzi wa vitabu hivyo umefanyika Novemba 15, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Watoto Njiti Duniani.

Akizungumza mara baada ya kuzindua vitabu hivyo, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, ameipongeza Doris Mollel Foundation kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha huduma za Afya ya Mama na Mtoto nchini, hususan huduma kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.

Amesema Serikali itaendelea kuimarisha huduma hizo kwa kuboresha miundombinu ya wodi maalumu, kuongeza upatikanaji wa huduma bora na kuhakikisha wazazi wanashirikishwa katika malezi ya watoto njiti tangu siku ya kwanza.

Akivitaja vitabu hivyo, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Doris Mollel Foundation, Doris Mollel, amesema vitabu vilivyozinduliwa ni “Nimejifungua Njiti, Nifanyeje?” kinacholenga kuwasaidia wazazi kukabiliana na changamoto za kupata mtoto njiti; Kitabu kinachotoa mwongozo wa huduma za kisaikolojia na kijamii kwa mama wa watoto njiti; pamoja na “Hivi Ndivyo Tunavyotaka Vitengo vya Huduma kwa Watoto Wachanga (NCU) Viwe” kinachotoa mwongozo kwa wazazi kuhusu muundo na mazingira ya vitengo vya huduma kwa watoto wachanga.

Ameeleza kuwa vitabu hivyo havitauzwa bali vitasambazwa kwa walengwa bure kwa lengo la kuongeza uelewa na kuboresha huduma kwa watoto njiti huku vikiwa na taarifa zilizozingatia uzoefu, changamoto na mahitaji halisi ya wazazi wenye watoto njiti, ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi mahitaji ya watoto na familia zao.

Uzinduzi wa vitabu hivyo ni sehemu ya juhudi za Serikali na wadau wa sekta ya afya katika kuboresha huduma na malezi ya watoto njiti, kupunguza vifo vya watoto wachanga na kuhakikisha wanapata nafasi salama ya kukua na kuendelea vizuri.

About the author

Alex Sonna