Featured • Kitaifa

NAIBU WAZIRI MHE.QWARAY AAGIZA WATUMISHI WAPYA KUPATIWA MAFUNZO NDANI YA MIEZI MITATU

Written by Alex Sonna

 

 

Na Lusungu Helela, Manyara

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray, amewaagiza waajiri katika taasisi za umma kuhakikisha watumishi wapya wanapatiwa mafunzo ya awali ndani ya miezi mitatu tangu kuajiriwa ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na maadili ya Utumishi wa Umma.

Mhe. Qwaray ametoa agizo hilo leo wakati wa kikao kazi cha kusikiliza na kujadili changamoto za watumishi wa umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara, ikiwa ni sehemu ya ziara zake za kikazi zinazolenga kuboresha utendaji katika Utumishi wa Umma.

Amesema waajiri wanapaswa kutenga bajeti kwa ajili ya mafunzo hayo, sambamba na kutenga fedha za kujikimu kwa ajira mpya, uhamisho na stahiki nyingine za watumishi.

“Watumishi wapya wapatiwe mafunzo ya awali ndani ya miezi mitatu tangu kuajiriwa, na waajiri watenge bajeti kwa ajili ya mafunzo hayo,” amesema Mhe. Qwaray.

Agizo hilo linatolewa wakati Serikali ikiendelea kuongeza idadi ya watumishi katika taasisi za umma ili kupunguza mzigo wa kazi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mhe. Qwaray amesema Serikali imeajiri watumishi 62,975 katika mwaka wa fedha 2025/2026 na inapanga kuajiri watumishi wengine 45,000 katika mwaka wa fedha 2026/2027.

Aidha, amezitaka mamlaka za ajira na nidhamu kusimamia haki na wajibu wa watumishi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma, huku akisisitiza umuhimu wa kuachana na utendaji wa mazoea.

Akizungumzia maadili ya Utumishi wa Umma, Mhe. Qwaray amewataka watumishi kuyafahamu na kuyatekeleza maadili yanayoongoza utendaji wao, ikiwemo kutoa huduma bora, kufanya kazi kwa uadilifu, kuheshimu sheria na kutoa huduma bila upendeleo.

Amesema mamlaka husika zinapaswa kuchukua hatua za kinidhamu kwa wakati dhidi ya watumishi wanaokiuka maadili au kutotekeleza majukumu yao ipasavyo.

Katika hatua nyingine, Mhe. Qwaray amewaagiza waajiri kushughulikia kwa wakati stahiki za watumishi, ikiwemo upandishaji vyeo, uhamisho, malimbikizo ya mishahara na mafao.

Vilevile, amewataka waajiri na mamlaka za ajira na nidhamu kushirikiana na Tume ya Utumishi wa Umma katika ukaguzi wa utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu za kiutumishi, pamoja na kurekebisha mapungufu yatakayobainika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Bi. Hawa Hassan, amesema mafunzo ya awali kwa watumishi wapya ni miongoni mwa vipaumbele vya halmashauri hiyo kutokana na mazingira ya kijiografia ya wilaya hiyo.

Bi. Hassan amesema halmashauri imeweka utaratibu wa kuwapatia mafunzo watumishi wapya, ikiwemo kuwaandaa kisaikolojia kutokana na changamoto za mazingira ya wilaya hiyo.

About the author

Alex Sonna