NA MWANDISHI WETU MBINGA, RUVUMA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameanza rasmi ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma kwa kutembelea Wilaya ya Mbinga vijijini, ambako amekagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi wa Kigonsera na Amani Makoro kuhusu masuala yanayogusa maisha yao, ikiwemo kilimo, miundombinu ya barabara, afya na maji na kuagiza NFRA kuhakikisha bei ya mahindi inamlinda mkulima kwa alichowekeza na sio kumkata
Mhe Ndejembi ameyasema hayo kufuatia hoja iliyowasilishwa na mbunge wa mbinga vijijini Mhe Judith Kapinga juu ya haja ya kuwafikiria wakulima wa Kigonsera juu ya bei ya mahindi ambayo imekuwa changamoto kwao na kumwelekeza NFRA kuhakikisha msimu ujao bei inakuwa ni ya kuridhisha na kuwalinda wakulima wa mahindi.

Aidha Mhe Ndejembi amesema kuwa mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa yenye kuzalisha kiasi kikubwa cha mahindi kwa kufanya hivyo itamlinda mkulima, italinda usalama wa chakula na kuweka uwiano mzuri wa bei kwa wakulima
Akizungumza wakati wa mkutano na wananchi wa Kigonsera Mbunge wa jimbo la Mbinga vijijini na Waziri wa viwanda na Biashara Mhe judith kapinga amesema halmashauri inatarajia kujenga eneo maalumu la kuhifadhi mahindi sambamba na kiwanda kwa ajili ya kumpunguzia adha mkulima kwenye ununuzi wa mahindi kitakachogharimu bilioni 7.83.
Awali makamu wa Rais ametembelea mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga na kupokea taarifa ya utekelezaji wake, ambapo imeelezwa kuwa kati ya majengo 29 yanayohitajika kwa mujibu wa mwongozo wa Serikali, majengo 15 yamekamilika huku 14 yakiwa bado hayajajengwa ambapo yaliyokamilika ni shilingi bilioni 3.62, ambapo shilingi bilioni 3.4 zimetolewa na Serikali Kuu na shilingi milioni 220 zimetokana na mapato ya ndani ya halmashauri.
Akizungumzia maendeleo ya mradi huo, Mhe. Ndejembi amesisitiza umuhimu wa halmashauri kutumia mapato yake ya ndani kutekeleza miradi yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi, badala ya kutegemea Serikali Kuu katika kila hatuna na kuelekeza halmashauri kutenga angalau shilingi milioni 200 kila mwaka kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi wa afya karibu na hospitali hiyo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma, hususan wakati wa usiku.
Akizungumza wakati wa ziara ya Mhe Makamu wa Rais Mbunge wa jimbo la Mbinga na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Judith Kapinga amesema tayari halmashauri imeelekeza kutengwa kwa shilingi milioni 300 katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mbili za watumishi zenye uwezo wa kuhudumia familia tatu kila moja (3 in 1), huku akieleza kuwa juhudi zinaendelea kutafuta namna ya kuongeza idadi ya nyumba zitakazojengwa ili watumishi waweze kuishi karibu na hospitali.
Katika mkutano na wananchi wa Kigonsera, Mhe. Kapinga ameeleza umuhimu wa sekta ya kilimo katika uchumi wa Mbinga, hususan uzalishaji wa mahindi na kahawa ambapo amesema wakulima wa maeneo hayo wanatumia nguvu kubwa kuzalisha mazao hayo, huku akiishukuru Serikali kwa hatua za kununua mahindi kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wakulima wananufaika na shughuli zao za uzalishaji kupitia upatikanaji wa soko la uhakika.
Ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kupeleka rasilimali katika maeneo mbalimbali ya Mbinga kwa ajili ya kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi, ikiwemo ujenzi wa hospitali, upatikanaji wa umeme, barabara, shule na maji nakusisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kuhifadhi mazingira kwa kutunza miti na misitu ili kulinda vyanzo vya maji na kuimarisha shughuli za kilimo.
Akizungumzia changamoto ya miundombinu ya barabara, Mhe. Ndejembi ameitaka Wizara ya Ujenzi kuandaa mpango kazi utakaoharakisha ukamilishaji wa barabara ya Amani Makoro–Ruanda, akisisitiza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha usafirishaji wa abiria na mazao, kupunguza changamoto za usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa Mbinga na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla na kuongeza kuwa Kama mkandarasi ameshindwa kukamilisha ujenzi huo atafutwe mkandarasi mwingine.
Aidha, amesisitiza kuwa barabara hiyo ya Amani makoro ni kiungo muhimu kwa usafirishaji wa makaa ya mawe usafirishaji wa mazao na kuomba kuwepo na kituo kimoja cha utoaji huduma eneo la mizani ili kuongeza mapato kwa wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga na Amani makoro .
Kwa upande wa huduma za maji, katika mazungumzo na wananchi wa Amani Makoro, Mhe. Kapinga ameishukuru Serikali kwa uwekezaji wa shilingi bilioni 1.6 katika mradi wa maji, akieleza kuwa mkandarasi tayari amepatiwa shilingi milioni 300 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, huku fedha nyingine zikitarajiwa kutolewa ili kuhakikisha kazi inaendelea na wananchi wananufaika na huduma ya maji.
Ziara hiyo ni sehemu ya shughuli za Makamu wa Rais za kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kusikiliza maoni na changamoto za wananchi, ikiwa ni pamoja na kufuatilia hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha huduma za afya, maji, usafiri na shughuli za kiuchumi katika Mkoa wa Ruvuma na alipata fursa ya kuzungumza na wananchi wa Kigonsera, Amani makoro na wananchi eneo la soko la songea mjini.