Featured • Kitaifa

MRADI WA HOMBOLO KUIBADILISHA DODOMA KUWA KITOVU CHA UTALII NA BURUDANI DUNIANI

Written by Alex Sonna
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA: 
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema ujenzi wa Mji wa Hombolo ni hatua muhimu katika kutimiza maono ya kuifanya Dodoma kuwa jiji la kimataifa, lenye kuvutia uwekezaji, utalii, burudani na fursa mbalimbali za kiuchumi.
Amesema mradi huo unaenda kuongeza thamani ya Jiji la Dodoma na kulipa sura mpya itakayoliwezesha kushindana na miji mikubwa duniani, huku ukichochea ongezeko la wageni na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.
Akizungumza leo Novemba 9, 2026, jijini Dodoma, wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa upembuzi yakinifu na uandaaji wa Mpango Kabambe wa Mji wa Kisasa wa Hombolo,Senyamule amesema alivutiwa na muonekano na dhana ya maendeleo ya Mji wa Hombolo, akieleza kuwa kwa kiwango cha ubunifu kilichooneshwa, mradi huo unaweza kuifanya Dodoma kutambulika kimataifa.
Ameeleza kuwa maendeleo ya Dodoma hayawezi kutegemea ongezeko la watumishi wa Serikali wanaohamia katika makao makuu pekee, bali yanahitaji uwekezaji mpana katika sekta za uzalishaji, utalii na huduma.
Amesema Mkoa wa Dodoma umeweka vipaumbele vya kiuchumi vinavyojumuisha kilimo, utalii, lojistiki, uwekezaji wa kimkakati, madini, viwanda na ujenzi, huku Mji wa Hombolo ukiwa sehemu ya utekelezaji wa mkakati huo kupitia sekta ya utalii.
BURUDANI KUVUTA WAGENI DODOMA
Senyamule amesema uwekezaji katika burudani na vivutio vya utalii ni miongoni mwa njia muhimu za kuvutia watu kutembelea na kutumia muda wao katika Jiji la Dodoma.
Ametoa mfano wa miji mikubwa kama Dubai, ambayo huvutia wageni kutokana na uwepo wa shughuli mbalimbali za uwekezaji, burudani na vivutio vya kipekee.
Amesema kupitia Mji wa Hombolo, Dodoma inatarajia kuwa na vivutio vitakavyowafanya watu kutoka maeneo mbalimbali duniani kuja kutembelea, kufurahia na hata kuchagua kuishi jijini humo.
Ameongeza kuwa uwepo wa vivutio hivyo utasaidia pia kuvutia mikutano mikubwa ya kimataifa, uwekezaji katika hoteli na huduma nyingine, hali itakayochochea ukuaji wa uchumi wa jiji.
PONGEZI KWA UONGOZI NA WATEKELEZAJI
Katika hatua nyingine, Senyamule amewapongeza viongozi wa Wilaya ya Dodoma, Jiji la Dodoma pamoja na wataalamu walioshiriki katika kubuni na kusukuma utekelezaji wa mradi huo.
Amempongeza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kwa kasi ya kutafsiri maono ya maendeleo kuwa hatua za utekelezaji, akieleza kuwa mradi huo ni miongoni mwa vipaumbele alivyowasilisha tangu alipokutana na uongozi wa jiji.
Amesema anaamini Mji wa Hombolo utakuwa sehemu muhimu ya kuonesha utajiri wa vivutio na maendeleo ya Tanzania, huku ukitoa fursa kwa wageni kuona taswira ya dunia kupitia uwekezaji unaofanyika ndani ya jiji hilo.
Amesisitiza kuwa mradi huo unaonesha namna ambavyo ushirikiano kati ya Serikali, viongozi na wataalamu unaweza kuleta matokeo makubwa katika kutekeleza mipango ya maendeleo.
Amesema anaamini Dodoma ina nafasi ya kuwa miongoni mwa miji bora barani Afrika na duniani, huku Mji wa Hombolo ukiwa sehemu ya safari hiyo ya kuifanya Dodoma kuwa jiji lenye hadhi ya kimataifa.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, amewataka washauri elekezi wa ndani na nje ya nchi kuhakikisha upembuzi yakinifu na uandaaji wa Mpango Kabambe vinakamilika kwa wakati, ikiwezekana kabla ya muda wa miezi sita uliopangwa.

Shekimweri amesema mafanikio ya mradi huo yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya wataalamu, viongozi na wadau wote, huku akiahidi kuwa Serikali itatoa ushirikiano unaohitajika ili kufanikisha kazi hiyo.

Awali, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko, amesema mradi wa Hombolo unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika taswira na maendeleo ya Dodoma, kwa kulitayarisha jiji kuwa la kisasa na lenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya kitaifa na kimataifa.

Amesema mradi huo ulianza safari yake mwishoni mwa mwaka 2024 na umehitaji muda wa maandalizi, tafiti na kujifunza ili kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa na ufanisi. Ameeleza kuwa muda uliotumika haukumaanisha kukosekana kwa dhamira, bali ulikuwa sehemu ya maandalizi ya mradi ambao ni mpya kwa Dodoma na maeneo mengi nchini.

Dkt. Sagamiko amesema ziara za mafunzo katika nchi mbalimbali, ikiwemo Korea, zimewasaidia viongozi na wataalamu kupata uzoefu wa utekelezaji wa miradi inayofanana na huo. Aidha, amesema taasisi za fedha zimeonesha utayari wa kushiriki katika uwekezaji, huku jiji likiwashirikisha taasisi za elimu ya juu, wadau wa Hombolo na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Amesema mradi huo unalenga kuimarisha hadhi ya Dodoma kama makao makuu ya nchi, kwa kuandaa mazingira yatakayowezesha jiji kupokea wawekezaji, wanadiplomasia na mikutano mikubwa ya kitaifa na kimataifa, sambamba na kukabiliana na changamoto za mipango miji na uwekezaji.

Amesisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaleta mabadiliko makubwa katika jiji hilo, akitumia kauli mbiu “Dodoma will never be the same again”, akimaanisha kuwa Dodoma haitakuwa kama ilivyo sasa baada ya mradi huo kukamilika.

Naye Mwenyekiti wa kampuni ya Heerim Architects and Planners, Young-in Jung, amesema kampuni hiyo italeta utaalamu wa kimataifa katika usanifu wa viwanja vya ndege, vituo vya mikutano, hoteli, makazi, biashara na mipango miji ili kuhakikisha Hombolo inakuwa mji wa kipekee wenye miundombinu ya kisasa.

Jung amesema kampuni hiyo ina uzoefu mkubwa katika miradi ya kimataifa na itatumia uwezo wake wote kuandaa mpango utakaowezesha maendeleo endelevu ya eneo hilo, huku ikizingatia viwango vya kimataifa, urithi wa eneo na uhifadhi wa mazingira.

Amesema maono ya mradi huo ni kuifanya Hombolo kuwa mji wa kijani na wenye teknolojia janja (Smart City), unaotarajiwa kuvutia wageni 500,000 kila mwaka na kuzalisha zaidi ya ajira 100,000 ifikapo mwaka 2045, hatua inayolenga kuimarisha uchumi na kuweka viwango vipya vya maendeleo endelevu nchini.

Kwa upande wake  Mratibu wa Mradi wa Hombolo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Timu ya Miradi katika Halmashauri ya Wilaya ya Dodoma Bw.Azori William,amesema mradi wa maendeleo ya mji wa Hombolo umebeba matumaini makubwa ya kuibadilisha Dodoma kuwa kitovu cha uchumi, biashara na utalii nchini Tanzania.

Akizungumza kuhusu mradi huo, ameeleza kuwa wazo la kuanzishwa kwake limetokana na kasi kubwa ya ukuaji wa Jiji la Dodoma kufuatia kuhamishwa kwa shughuli za Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, hali iliyochochea ongezeko la mahitaji ya ardhi, makazi, huduma za kijamii na maeneo ya uwekezaji.

Amesema mradi huo unalenga kuifanya Dodoma kuwa jiji lenye uwezo wa kuwahifadhi wakazi na wageni wake kwa kuwapatia fursa mbalimbali za kiuchumi, biashara, ajira na huduma bora badala ya kuwa jiji ambalo watu wengi hulitumia kwa shughuli za kikazi pekee.

Kwa mujibu wake, mradi huo umebuniwa kwa kuzingatia dhana mbalimbali za kimataifa, ikiwemo Country Within the City, inayolenga kuifanya Hombolo kuwa na vivutio vinavyowakilisha maeneo mbalimbali ya utalii nchini Tanzania, pamoja na dhana ya Global Village, itakayowezesha kuonesha tamaduni, vyakula, mavazi na usanifu wa majengo kutoka mataifa mbalimbali yenye uhusiano na Tanzania.

Katika kuimarisha hadhi ya Hombolo, William amesema mji huo unapangwa kuwa Smart City, utakaotumia teknolojia za kisasa kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, kuimarisha usafiri na kuongeza ufanisi wa matumizi ya nishati.

Aidha, amesema mradi umezingatia dhana ya mji endelevu, salama na rafiki kwa mazingira, ambapo zaidi ya asilimia 50 ya eneo linaloendelezwa linatarajiwa kutengwa kwa shughuli za kijani ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, joto kali na mafuriko.

Dira hiyo pia inajumuisha matumizi ya nishati jadidifu, hususan nishati ya jua, pamoja na mifumo mbalimbali ya usafiri inayolenga kurahisisha maisha ya wakazi.

Amefafanua kuwa mradi huo unatarajiwa kutekelezwa katika eneo lenye ukubwa wa takribani ekari 24,000, likiwa na fursa ya kuunganisha miundombinu muhimu ya kimkakati ikiwemo Uwanja wa Ndege, Mji wa Serikali na eneo la Bandari Kavu ili kuunda mfumo mmoja jumuishi wa maendeleo.

Amesisitiza kuwa uwepo wa Bwawa la Hombolo, lenye ukubwa wa takribani ekari 1,500, ni moja ya rasilimali muhimu zinazotarajiwa kuupa mji huo upekee kupitia mradi wa Waterfront Development, utakaolenga kuendeleza maeneo ya pembezoni mwa bwawa kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira huku ukifungua milango ya uwekezaji katika hoteli, burudani, utalii na shughuli nyingine za kiuchumi.

Kuhusu utekelezaji, William amesema Halmashauri imejipanga kutumia mfumo wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP), kwa kushirikisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, taasisi za kifedha na wadau wa maendeleo.

Amesema tayari mradi umewasilishwa kwa wadau mbalimbali na kupokea mwitikio mkubwa, huku baadhi ya wawekezaji wakionesha nia ya kuanzisha miradi ya kimkakati ikiwemo vituo vya usafirishaji na huduma za ugavi (Logistics Hub).

Ameongeza kuwa uzoefu kutoka katika miji mingine duniani unaonesha umuhimu wa kuwashirikisha wananchi katika miradi mikubwa ya maendeleo, hivyo Halmashauri imeweka msisitizo wa kuhakikisha wananchi wanakuwa sehemu ya maandalizi na utekelezaji wa mradi huo ili wanufaike moja kwa moja na fursa zitakazojitokeza.

 Amesema mradi huo si mpango wa kujenga mji wa kisasa pekee, bali ni mkakati mpana wa kuipa Dodoma sura mpya ya kimataifa, kuongeza fursa za ajira na uwekezaji, kukuza utalii na kuboresha maisha ya wananchi. Hombolo inalenga kuwa zaidi ya makazi; inakusudiwa kuwa alama mpya ya maendeleo ya Dodoma na kitovu cha fursa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

About the author

Alex Sonna