Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akizungumza jambo katika eneo la Tura, mkoani Tabora wakati wa ziara yake ya siku mbili ya kukagua Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), katika vipande vya Tatu, Nne na Tano, akiambatana na Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani).
Na. Joseph Mahumi na Asia Singano, WF, Tabora
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, amewataka wakandarasi wanao jenga Reli ya Kisasa (SGR) kuongeza kasi ili kufidia muda uliopotea kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza, na kuzingatia ubora wa kazi na masuala ya mazingira na jamii.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua na kujionea maendeleo ya ujenzi wa Reli ya Kisasa(SGR), katika vipande vya tatu, nne na tano, Mhe. Balozi Omar alisema Serikali inataka kuona mradi huo unatekelezwa kwa kasi zaidi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kuunganisha maeneo mbalimbali ya nchi kwa njia ya reli ya kisasa.
Alisema pamoja na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mradi huo na zilizoelezwa na mkandarasi, mshauri Melekezi pamoja na Shirika la Reli Tanzania (TRC), Serikali imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutafuta suluhisho litakalowezesha kuharakisha maendeleo ya ujenzi.
Mhe. Balozi Omar aliipongeza TRC, Wizara yake nawataalamu wengine walioshiriki kubuni utaratibu mbadala uliosaidia kuondoa baadhi ya vikwazo na kuimarisha kasi ya utekelezaji wa mradi huo.
“Kwa mujibu wa taarifa, utekelezaji wa kipande hiki cha Tatu umefikia asilimia 16.1, na kipande cha Nne asilimia 10.08, ni maendeleo mazuri, ingawa juhudi zaidi zinahitajika ili kuongeza kasi na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati” alisema Mhe. BaloziOmar
Alibainisha kuwa ujenzi wa reli hiyo una umuhimu wa kimkakati katika kuunganisha maeneo ya mashariki na magharibi mwa Tanzania, kuanzia Dar es Salaam kupitia Dodoma hadi Mwanza na kuendelea kuelekea Kigoma.
Alisema Serikali na washirika wake wa maendeleo wanapaswa kuhakikisha masuala hayo yanashughulikiwa mapema badala ya kusubiri hadi changamoto zijitokeze wakati wa utekelezaji au baada ya fedha za mradi kutolewa.Mhe. Balozi Omar alihimiza kuendelea kwa ushirikiano wa karibu kati ya Wizara ya Fedha, TRC, wakandarasi, washauri elekezi na wataalamu wengine ili kuhakikisha mradi wa SGR unakamilika kwa ufanisi na kutoa mchango uliokusudiwa katika kukuza uchumi, kurahisisha usafirishaji na kuimarisha maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, amesema ziara ya pamoja na Waziri wa Fedha katika Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) imelenga kuimarisha ushirikiano kati ya wizara hizo mbili katika kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo zinatumika ipasavyo.
Alisema ni muhimu Wizara ya Fedha, ambayo inasimamia upatikanaji wa fedha, kujionea maendeleo ya miradi inayofadhiliwa, huku Wizara ya Uchukuzi ikiendelea kusimamia utekelezaji wake.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Machibya Shiwa, na Mhandisi Mshauri mradi, Bw. Salim Omary Salim, wameeleza hatua zinazochukuliwa na shirika hilo pamoja na wasimamizi wa mradi katika kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi, sambamba na kuhakikisha utekelezaji unaendeleakufanyika kwa kuzingatia masharti ya kimkataba, viwango vyaubora na matakwa ya kimazingira ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa viwango vinavyotakiwa

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), (katikati), Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (wa pili kulia), wakikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, Kipande cha Nne – Tabora hadi Isaka (Km 165), ambacho hadi sasa kimefikia asilimia 10.08, wakati wa ziara yake ya siku mbili ya kukagua Mradi wa Ujenzi wa SGR, katika vipande vya Tatu, Nne na Tano, mkoani Tabora. Wengine katika picha ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya (kushoto), Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Machibya Shiwa (wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Miundimbinu Wizara ya Uchukuzi, Mhandisi. Shomari Omar Shomari
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), (wa kwanza kushoto), akisikiliza maelezo ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Machibya Shiwa, kuhusu maendeleo ya Mradi huo katika Kipande cha Tatu – Makutupora hadi Tabora (Km 368, wakati wa ziara yake ya siku mbili ya kukagua Mradi wa Ujenzi wa SGR, katika vipande vya Tatu, Nne na Tano, mkoani Tabora, akiambatana na Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya na Viongozi na Maafisa waandamizi wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Uchukuzi na Shirika la Reli Tanzania -TRC (hawapo pichani).

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), (wakwanza kushoto), akisikiliza maelezo ya Kiongozi wa Timu ya Ukandarasi wanaojenga Kipande cha Nne – Tabora hadi Isaka (Km 165), Bw. Sinan Doymus, kuhusu maendeleo ya Mradi huo ambao hadi sasa umefikia asilimia 10.08, wakati wa ziara yake ya siku mbili ya kukagua Mradi wa Ujenzi wa SGR, katika vipande vya Tatu, Nne na Tano, mkoani Tabora, akiambatana na Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya na Viongozi na Maafisa waandamizi wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Uchukuzi na Shirika la Reli Tanzania -TRC (hawapo pichani).
(Picha na Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini, WF -Tabora)