********
Kituo cha Uwekezaji Tanzania kwa kushirikiana na Ubalozi wa China nchini Tanzania wamefanya mkutano na Wawekezaji pamoja na wafanyabiashara wa China uliolenga kujadili masuala ya upatikanaji wa vibali vya kufanya kazi, ukaazi na upatikanaji wa cheti cha motisha kinachotolewa na Kituo cha Uwekezaji hapa nchini.
Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TIC Makao Makuu na kupitia zoom uliweza kuvutia zaidi ya wawekezaji 100 walioweza kufuatilia mkutano huo leo tarehe 5 Julai, 2022.
Kikao kiliongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, ndugu John Mnali na kuhudhuriwa na viongozi wa Taasisi zinazotoa vibali hivyo ikiwemo Kamishna wa Uhamiaji anaeshughulikia Vibali, Viza na Pasi, Kamishna Mary Palmer na Kamishna wa Kazi Msaidizi anaeshughulikia Vibali vya Kazi, Kamishna Msaidizi Lilian Fransis.
Akizungumza katika mkutano huo ndugu Mnali alisema TIC imejidhatiti kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji hapa nchini kwa kushirikiana na wawekezaji kuziainisha, kuzijadili na kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo ili kuhakikisha miradi ya uwekezaji haikwamishwi kwa ukosefu wa vibali mbalimbali.
Naye kamishna wa Uhamiaji Vibali Bi. Mary Palmer aliwasisitiza wafanyabiashara na wawekezaji kutoka China kuhakikisha kuwa wanafuata taratibu na misingi iliyowekwa ili kuweza kukamilishiwa upatikanaji wa vibali vya ukaazi ili kuepukana na changamoto mbalimbali zinazoweza kuwapata kutokana na kutokuwa na vibali sahihi.
Kamishna Msaidizi wa Kazi Bi. Lilian alisema Kamisheni ya kazi itaendelea kutoa
elimu kwa wawekezaji na wafanyabiashara hao ili kuhakikisha kwamba wanafuata taratibu katika kuomba na kupata vibali vya kazi hapa nchini. Alisema Idara ya kazi ipo tayari kuwasaidia wakati wote wanapokwama ili kuondoa usumbufu na urasimu.
Ndugu Mnali aliahidi kuitisha kikao kingine ambacho kitajadili zaidi masuala mengine yenye changamoto katika utekelezaji wa miradi hapa nchini.
Kituo cha Uwekezaji Tanzania kitaendelea kushirikiana na Taasisi mbalimbali za Serikali zinazotoa huduma chini ya Kituo cha Mahala Pamoja ili kuhakikisha kuwa changamoto zinazowakabili wawekezaji zinatatuliwa kwa wakati aliongeza Ndg. Mnali.