Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (kulia) akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Qatar Mhe. Habibu Awesi Mohamed, katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, Doha, Qatar, ambapo Mhe. Balozi Omar, anaongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa 11 wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Uwekezaji wa Miunombinu ya Asia (AIIB), unaofanyika nchini humo.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (katikati), Balozi Tanzania nchini Qatar Mhe. Habibu Awesi Mohamed (kulia), na Mkuu wa Utawala wa Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar, Bi. Maryam Haji Mrisho, wakiwa katika picha ya pamoja katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, Doha, Qatar, ambapo Mhe. Balozi Omar, anaongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa 11 wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Uwekezaji wa Miunombinu ya Asia (AIIB), unaofanyika nchini humo.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Doha, Qatar)
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar aimesisitiza umuhimu wa Serikali kufanya mapitio ya kimkakati katika matumizi ya rasilimali za mafuta na gesi ili kuleta tija zaidi kwa wananchi na bara la Afrika kwa ujumla.
Mhe. Balozi Omar amesema hayo wakati akiongoza kikao cha maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 11 wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Uwekezaji wa Miunombinu ya Asia (AIIB), , unaofanyika Doha nchini Qatar, kikao kilichofanyika katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini humo.
Alibainisha kuwa wakati umefika kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika zenye rasilimali hizo, kama Msumbiji, kuanza kufikiria namna ya kutumia gesi asilia kuzalisha mbolea kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya ndani badala ya kutegemea zaidi soko la nje.
Mhe. Balozi Omar alieleza kuwa matukio ya kimataifa, ikiwemo changamoto za usafirishaji katika mifereji mikuu ya dunia kama Strait of Hormuz, Suez na Panama, yametoa funzo kwa mataifa ya Afrika kuwa na utegemezi mdogo wa masoko ya kimataifa na badala yake kuimarisha uchumi wa ndani.
Kuhusu ajira, ilibainishwa kuwa ni jambo la faraja kuona Watanzania wengi wakipata ajira za staha nchini humo, huku kukiwa na takwimu zinazoonyesha kuwepo kwa Watanzania zaidi ya 2,500 katika maeneo hayo.
Aidha, alisisitiza haja ya kujifunza zaidi kutoka kwa mataifa ya Mashariki ya Kati kuhusu uchumi wa kemikali za mafuta, akibainisha kuwa ingawa Tanzania ilijifunza mengi kutoka Norway kupitia programu ya Oil for Development, sasa ni wakati wa kupanua wigo wa maarifa ili kuimarisha uchumi wa Taifa.
Aliupongeza Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar kwa kutimiza na kuadhimisha miaka 10 ya uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi na nchi hiyo, hatua ambayo alisema ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na maendeleo ya sekta ya nishati na sekta nyingine nchini.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Qatar Mhe. Habibu Awesi Mohamed, alisema Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Qatar umeendelea kuimarika tangu kuanzishwa kwa ubalozi huo mwaka 2017.
Alibainisha vipaumbele saba vinavyoongoza utendaji wa ubalozi huo katika kukuza maslahi ya Taifa ikiwemo kuimarisha diplomasia, masuala ya uchumi, kuvutia mitaji ya moja kwa moja (FDI), utalii, ajira, masuala ya diaspora, na elimu ya juu.
Kuhusu ajira, Mhe. Balozi Mohamed alisema kuna takriban Watanzania 2,500 wanaoishi na kufanya kazi nchini Qatar yenye jumla ya wakazi milioni 3 huku raia wake wanaoishi nchini humo ni laki tatu na kwamba mafanikio makubwa yameonekana katika sekta ya usafirishaji ambapo Watanzania 720 wameajiriwa kama madereva wa mabasi makubwa ya kampuni ya serikali.
Alisema kuwa Qatar, ambayo uchumi wake unategemea bidhaa za petroli kwa asilimia 85, inatazamwa kama chanzo muhimu cha mbolea kwa Tanzania, na kwamba Serikali inaendelea na mkakati wa kuona namna bora ya kupata mbolea kutoka nchini humo.
